Waliotoka Baraza la Wawakilishi wataja bandari na Katiba

Dodoma. Wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) ambao wameapishwa, wametaja mambo mawili kuwa watahangaika nayo na hawatakuwa mabubu.

Mambo hayo ni bandari, usafiri wa pamoja na uundwaji wa mfuko wa pamoja wa fedha ili kuondoa walichosema ni kelele za muda mrefu.

Wametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili Mosi, 2026 dakika chache baada ya kula kiapo cha utii na uzalendo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge sita wameapishwa wakiwemo watano kutoka Baraza la Wawakilishi ambao ni Fatuma Ramadhan Mohamed, Mariam Said Hamis, Shaame Ali Ali, Simai Mohamed Said (CCM) na Saidi Ali Mbarouk (ACT Wazalendo), wakati Dk Lazaro Bunungu ameapishwa akiwakilisha Jimbo la Peramiho (CCM).

Katiba ya Tanzania imetoa nafasi tano ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa sehemu ya wabunge katika Bunge la Tanzania bara.

Mwakilishi wa Gando, Said Ali Mbarouk amesema kazi kubwa itakayokuwa mbele yake ni suala la uundwaji wa mfuko wa pamoja wa fedha kwa kuwa anaamini ndiyo kilio cha walio wengi.

Mbarouk amesema changamoto hiyo haijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu lakini jambo hilo linapaswa kufikia mwisho tena mwisho uwe mwema.

“Changamoto kubwa ni uundwaji wa mfuko wa pamoja wa fedha, hilo sitolinyamazia, na ili kulimaliza linapaswa kuongozwa kwenye Katiba mpya ambayo itabeba mambo mengi,” amesema Mbarouk.

Kwa upande wake Simai Mohamed Said amesema lengo la kuingia bungeni kupitia Baraza la Wawakilishi ni kutaka apaze sauti ya kuunganisha Taifa liwe moja na watu wajenge utamaduni wa kutobaguana.

Amesema suala la bandari na usafiri wa pamoja ni muhimu vikaangaliwa kwani inawezekana kuwafanya Watanzania kuwa wamoja ambao hawatakuwa na kauli za kibaguzi.

“Kumekuwa na shida kidogo kwamba, Zanzibar inawahudumia watu wa huko pekee, hili siyo kwani ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila mtu ana haki sawa. Mahali popote hasa kwenye suala la kutumikiwa,” amesema Simai.

Amesisitiza ujio wake ndani ya Bunge hatakuwa bubu badala yake atakuwa balozi mwema wa kufikisha kilio cha Wazanzibar kwa kuzungumza na kutumia majukwaa mengine ikiwemo mazungumzo na Waziri Mkuu.