Dar es Salaam. Licha ya maendeleo yaliyopatikana katika ujumuishaji wa kifedha nchini, wanawake bado wanakosa uwakilishi wa kutosha katika nafasi za uongozi na uamuzi ndani ya sekta ya benki, jambo linalopunguza ubunifu na ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Aprili 1, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) Geofrey Mchangila wakati akizungumza kwenye jukwaa la wanawake lililoandaliwa na umoja huo.
Mchangila amesema licha ya jitihada zilizofanywa na benki mbalimbali kusaidia wanawake kupata mikopo na huduma za kifedha, pengo la kijinsia bado ni kikwazo kikubwa kinachoweza kuathiri ujumuishaji wa kifedha na kipato cha wanawake.
“Wanawake wanapewa mikopo na fursa, lakini bado hatuna uwakilishi wa kutosha katika nafasi za uongozi ndani ya benki. Hii inasababisha baadhi ya sera na maamuzi kushindwa kuakisi mahitaji ya wanawake kikamilifu,” amesema Mchangila.
Mchangila ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Citi Bank amesema kwa taasisi za fedha kutoa ahadi za sera pekee hakutoshi, bali benki zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kuboresha ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi, kuongeza uwakilishi wao katika bodi za maamuzi na kuhamasisha fursa za kifedha zinazolenga kundi hilo.
Mchangila ameongeza kuwa wanawake wanapopewa nafasi sawa za kushiriki katika maamuzi, ubunifu unaibuka na uchumi unapata nguvu zaidi kutokana na ukuaji wa kipato cha familia na jamii kwa ujumla.
Mkuu wa kitengo cha bidhaa Exim Bank Tanzania, Mtenya Cheya, akizungumza wakati wa jukwaa la wanawake lililoandaliwa na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kujadili ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya benki.
Aidha, amewataka wadau wa sekta ya benki kuunda mpango madhubuti wa utekelezaji wa sera za ujumuishaji wa kijinsia, unaolenga sio tu kutoa mikopo bali pia kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi ya kifedha.
“Tanzania imepiga hatua kubwa kupunguza pengo la kijinsia katika ujumuishaji wa kifedha, kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi tatu mwaka 2020. Hii ni matokeo ya mageuzi makusudi na utendaji wa taasisi za kifedha.
“Tunahitaji benki zote kuchukua hatua za vitendo ili kuziba pengo la kijinsia. Ni wakati sasa wa kufanya zaidi kuliko kutoa ahadi tu,” amesema Mchangila, akisisitiza umuhimu wa hatua zinazolenga kuboresha usawa wa kijinsia katika sekta ya kifedha.
Akizungumza kwenye jukwaa hilo, Mkuu wa kitengo cha bidhaa Exim Bank Tanzania, Mtenya Cheya amesema kukuza ujumuishaji wa kifedha kunahitaji muundo maalum wa bidhaa na ahadi thabiti ya taasisi badala ya kauli za sera za jumla.
“Benki lazima ziende zaidi ya kutoa huduma za kawaida na badala yake zitatengeneza suluhisho linalowakilisha hali halisi ya wanawake, ikiwemo ukosefu wa dhamana, mapato yasiyo ya kawaida, na uwiano kati ya biashara na familia,” amesema Mtenya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji TBA, Tuse Joune, amesema elimu ya kifedha imeanza kuwaletea mabadiliko wanawake, wengi wakijua sasa wapi wanaweza kupata mikopo kutoka taasisi zinazotambulika.
“Baada ya kutoa elimu ya kifedha, malalamiko kuhusu mikopo isiyo rasmi yamepungua kwa sababu wanawake wamepokea maarifa sahihi na sasa wanajua wapi wawekezaji,” amesema Tuse.