Watendaji ardhi kupimwa kwa migogoro waliyoitatua

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha migogoro ardhi inafikia kikomo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeelekezwa kupima utendaji kazi wa watumishi wake kwa idadi ya changamoto za migogoro ya ardhi wanayoitatua na hati wanazozitoa.

Mbali na hilo, wizara hiyo imeelekezwa hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watumishi wote watakaobainika kuwa chanzo cha migogoro hiyo na kuhakikisha taratibu na mifumo inayotumika katika kutoa huduma za ardhi, inakuwa ya wazi na rafiki kwa wananchi wote.

Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatano Aprili Mosi, 2026 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Sh12.5 trilioni ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni jijini Dodoma.

Kabla ya kutoa maelekezo hayo, Dk Mwigulu amesema sekta ya ardhi ni muhimu katika kuwezesha uzalishaji na maendeleo ya sekta nyingine. Hata hivyo, sekta hiyo imekumbwa na changamoto na migogoro mbalimbali.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na maeneo mengi kutopimwa, ucheleweshaji wa utoaji wa hati, umilikishaji wa eneo moja kwa zaidi ya mtu mmoja na baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu.

“Changamoto hizo zimesababisha uwepo wa migogoro baina ya makundi mbalimbali katika jamii yakiwemo ya wakulima na wafugaji sambamba na migogoro ya mipaka baina ya vijiji,” amesema Dk Mwigulu.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema Serikali imeendelea kutatua migogoro iliyopo kupitia kliniki za ardhi, kamati za wataalamu, mabaraza ya ardhi na ziara za viongozi.

“Hadi Januari, 2026 migogoro 5,333 imetatuliwa, maombi ya umiliki 10,113 yalipokelewa na hatimiliki 7,182 ziliandaliwa pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 191.

 “Ninaelekeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha mifumo ya kushughulikia migogoro ya ardhi. Pia, kuendelea kutatua changamoto zilizopo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kuimarisha matumizi ya Tehama,” amesema.

Hivi karibuni, katika ziara alizofanya katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Rukwa, miongoni mwa kero kubwa alizokutana nazo ni ya migogoro ya ardhi ambapo watu wenye kipato cha juu kudaiwa kutumia nafasi na ushawishi wao kuwanyang’anya haki wenye kipato duni.

Kutokana na kukithiri kwa malalamiko kuhusu migogoro ya ardhi, Dk Mwigulu aliwaagiza wakuu wote wa mikoa, kufanya uchunguzi katika maeneo yanayolalamikiwa na kuchukua hatua.

Ni migogoro hiyo ya ardhi, ndiyo iliyomsababisha Dk Mwigulu alipokuwa Sumbawanga Mjini, Mkoa wa Rukwa kuwataka viongozi na mawaziri wa kisekta kutafakari na kupendekeza mbinu itakayoleta suluhu ya kudumu.

Waliopewa jukumu hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Hamza Johari, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndejembi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe.