NCC yaja na mbinu kukabili migogoro sekta ya ujenzi

Dar es Salaam. Ili kuharakisha umalizaji wa migogoro katika sekta ya ujenzi, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) linaendesha mafunzo ya utatuzi wa migogoro nje ya mahakama kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Hatua hiyo inaelezwa itasaidia kupatikana kwa suluhu ya haraka kwa migogoro inayoibuka katika sekta hiyo, hivyo kuchangia kazi za ujenzi ziendelee na kumalizika kwa wakati.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 27, 2024 wakati akitoa mafunzo hayo   yanayoratibiwa na NCC, Mkadiriaji Majenzi wa baraza hilo, Elias Kissamo, amesema wanaamini mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuwa na uelewa mpana wa njia bora za kutatua migogoro katika shughuli zao, badala ya kupelekana mahakamani. Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza Juni 26, mwaka huu.

Amesema baraza hilo limeundwa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini, ikiwemo kusaidia kuwapo kwa njia sahihi za kusimamia usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama.

“Baraza linasimamia usuluhishi wa migogoro katika sekta ya ujenzi na si msuluhishi, miongoni mwa majukumu yake ni kuchagua wasuluhishi miongoni mwa waliopo kwenye mpangilio, ili washughulike na utatuzi wa mgogoro unaopaswa kutatuliwa,” amesema Kissamo.

Kwa upande wake, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Fauz Twaib, amesema kutokana na kuwepo migogoro imeonekana kuna haja ya kuwapo mfumo mbadala wa mahakama kutatua migogoro hiyo.

Dk Twaib ambaye pia ni Rais wa Chama Cha Mawakili Afrika Mashariki, amesema kuna mambo mengi yanayoweza kuepukwa kwa kutumia mfumo nje ya Mahakama.

“Migogoro mahakamani inachukua muda mrefu, jambo hili litasaidia migogoro kutatuliwa kwa haraka, ili kazi za ujenzi zimalizike kwa wakati.

“Pia hatua hii itasaidia kupunguza matumizi ya muda mahakmani, gharama mbalimbali pamoja na kuwaacha wahusika katika uhusiano mwema,” amesema.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali, Rehema Mtulya, amesema mafunzo yatamsaidia kuendesha mashauri ya usuluhishi kwa weledi zaidi.

Related Posts