NYOTA wa zamani wa Yanga aliyekuwa akikipiga Al Murooj ya Libya, Heritier Makambo anatajwa kuanza mazungumzo na Tabora United ili ajiunge na timu hiyo iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita.
Inadaiwa kuwa mazungumzo ya pande hizo mbili yanaendelea vyema na huenda akatua nchini.
WINGA wa zamani wa Azam FC, Ayoub Lyanga anatajwa kuwindwa na KenGold baada ya dili la awali la kutakiwa na Simba kuonekana kuota mbawa.
Inadaiwa mbali na KenGold, lakini nyota huyo wa zamani wa Coastal Union anawindwa pia na Wagosi na Pamba Jiji, huku KMC nayo ikitajwa.
KLABU ya Simba inadaiwa kupambana kupata saini ya mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Yao Jean Charles Olivier ambaye yupo huru.
Nyota huyo amemaliza mkataba na SKA Khabarovsk ya Russia jambo linalowafanya mabosi wa Msimbazi kuanza kumpigia hesabu ili akaongeze nguvu eneo la ushambuliaji.
BEKI wa kati wa Simba, Hussein Kazi anajiandaa kutua Fountain Gate kwa mkopo baada ya mabosi wa Msimbazi kuamua kumpunguza kikosini ili kumpisha Abdulrazak Hamza aliyetambulishwa majuzi.
Kazi mkataba wake na Simba ni hadi mwakani, lakini mabosi wameamua kumtoa kwa mkopo.
NYOTA wa zamani wa Simba aliyekuwa Coastal Union, Haji Ugando inadaiwa ameachana na timu hiyo na sasa anajiandaa kuibukia KenGold iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
Ugando alikuwa kati ya wachezaji walioipa Coastal tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini amemaliza mkataba.