BENKI ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imekabidhi gawio la Sh bilioni saba kwa mwanahisa wake wa pekee Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2023. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inamiliki asilimia 100 ya hisa za benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, Arafat Haji alikabidhi gawio hilo kwa Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango – Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum aliyewakilisha serikali ya SMZ wakati hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika jana Jumamosi kwenye Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya PBZ, Mpirani, Zanzibar. Hafla hiyo ilienda sambamba na Mkutano wa Mwaka wa Wanahisa (AGM).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dk. Mkuya pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2023, aliwasilisha salamu za Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ally Mwinyi ambaye pia aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio litokanalo na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.
“Serikali inafurahishwa na mafanikio mnayoendelea kuyapata na msisitizo wetu kwenu nyinyi kuedelea kujiendesha kwa ufanisi na uweledi. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda.

“Gawio hilo la 7 bilioni ambalo Serikali imelipokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati. Hivyo naipongeza sana kwa mafanikio haya…hongereni sana,’’ alisema Dk. Mkuya.
Awali akizungumza kwenye tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa BPZ, Joseph Meza alieleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo unathibitisha imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa benki hiyo.
“Tuna furaha kusalia katika dhamira yetu ya kufikia malengo yetu muhimu katika kupanua nyayo zetu na kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha uzoefu wa wateja wetu.
“Leo, tunafurahi kukabidhi hundi ya Sh 7 bilioni kama gawio kwa mwaka 2023. Tunatazamia mustakabali wenye matumaini zaidi huku pia tukiwa tunaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu,” alisema Meza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, Arafat Haji aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa taasisi za fedha kama Benki ya PBZ kustawi huku pia akiipongeza Bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa jitihada kubwa walioifanya hadi kufikia mafanikio hayo.
“Utendaji kazi wa Benki unaonyesha mazingira bora ya biashara ambayo yalituruhusu kuwafikia wateja wetu kwa urahisi. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua nyayo zetu na kuboresha huduma zetu ili kukidhi na kuzidi matarajio ya wateja wetu.” Alisema Haji.
Ndani ya Mwaka 2023, PBZ Bank ilifanikiwa kukuza faida yake hadi kufikia Sh 74 Bilioni kabla kodi huku rasilimali zikiongezeka hadi kufikia Sh Trilioni 2.05.
Kwa mujibu Haji benki hiyo yenye matawi 33 ipo kwenye mkakati wa kuongeza matawi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini huku tayari ikiwa imefungua matawi kwenye mikoa ya Morogoro na Mbeya hivi karibuni.