RITA yazifilisi rasmi Sasatel, kampuni ya Hydrox

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imetangaza kuzifilisi Kampuni za DOVETEL (T)LIMITED maarufu kama Sasatel na Kampuni Hydrox Industrial Serivices Limited baada ya kujiridhisha kuwa kampuni hizo mbili zimeshindwa kujiendesha na kulipa madeni waliyonayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana Jumapili kutoa ufafanuzi kuhusu hatua hiyo iliyofikiwa ya kuzifilisi kampuni hizo, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi alisema hatua hiyo inalenga kulinda haki za wanahisa, wabia, wadeni, wafanyakazi na pia kuwezesha kodi na toto mbalimbali za serikali kulipwa ipasavyo.

Kabidhi Wasii Mkuu ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Bw. Frank Kanyusi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kutolea ufafanuzi kuhusu matangazo yaliyotolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhusu kuzifilisi Kampuni za DOVETEL (T)LIMITED maarufu kama Sasatel na Kampuni Hydrox Industrial Serivices Limited jana Jijini Dar es Salaam.

“Ningependa umma wa watanzania ufahamu kuwa RITA mbali ya kusajili vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto wa kuasili pia katika ufilisi tunaangalia usimamizi wa makapuni na ufilisi wa makampuni na watu binafsi pamoja usajili wa bodi za wadhamini, kusimamia mali isiyokuwa na mwenyewe, kuandika na kutunza wosia sambamba kusimamia mirathi,” alisisitiza Kanyusi.

Alisema RITA imeshapewa idhini na mahakama ya kuzibinafsisha kampuni hizo na kutoa matangazo katika vyombo vya habari kuutangazia umma na hasa wale wote ambao wana maslahi yeyote katika kampuni hizo kujitokeza kabla ya kukamilisha mchakato wa ubinafsishaji.

“Kazi ya ufilisi nchini inaongozwa na sheria mbalimbali kutegemeana na biashara inayofanywa na Kampuni inayofilisiwa. Sheria hizo ni Pamoja na Sheria na Ufilisi Sura ya 25, Sheria ya Makapuni ya mwaka 2012, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha Sura ya 342, Sheria ya Vyama vya Ushirika sura ya 211, Sheria ya Bima 394, Sheria ya Mashirika ya Umma, Sheria ya Hati za Makubaliano na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318,” alisema.

Kanyusi amesema RITA imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kufikia matarajio na malengo ya Seruikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa ya R nne(4Rs) yaani Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu  na Ujenzi mpya.

Akifafanua zaidi, Kanyusi alisema kwamba ufilisi wa kampuni hizo ni hatua muhimu kwani endapo kampuni hizo zitaachwa bila kufilisiwa mali zake zinaweza kutoweka wakati makundi tajwa yatapoteza haki zake za kisheria.

Kampuni ya DEVETEL au Sasatel ilianzishwa kwa nia ya kufanya biashara ya mawasiliano na ile ya kampuni ya Hydrox Industrial Services Limited ilikuwa ikijihusisha na kuzalisha na kuuza madawa na kemikali za kusafisha maji.

Related Posts