Makonda: Vyombo vya ulinzi, usalama vitokomeze rushwa

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani hapa kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa na kulindana ndani yao kwa kuwa madhara yake ni makubwa.

Amesema vyombo hivyo vinapaswa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwabaini watendaji wenzao kwenye taasisi wanaokiuka maadili na kuwa kabla hawajafanya operesheni mitaani waanze ndani ya taasisi zao.

Amesema ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi, kuanzia Agosti mosi, mwaka huu, lita 20,000 za mafuta ya gari zitakuwa zikitolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Arusha, vitakavyosaidia doria na kutoa huduma ikiwemo ya zimamoto.

Makonda ameyasema hayo leo Alhamisi, Julai 11, 2024, jijini Arusha akizungumza katika kikao na vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Arusha, kilicholenga kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama na ushirikiano na vyombo vya habari.

Amesema suala la rushwa linahitaji ushirikiano wa taasisi zote na kuwa Takukuru pekee haiwezi kutokana na suala hilo kutokuwa na dini au kabila.

Amesema katika baadhi ya taasisi, shughuli zimekuwa zikikwama kutokana na baadhi ya watendaji kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa endapo watafanya kazi kama timu kwa kushirikiana wataweza kumaliza vitendo hivyo.

“Kuna kipindi nilikuwa napata taarifa kwamba madini yanapelekwa kwa pikipiki na watu wanayavusha ng’ambo ya pili wanaenda kuuza kule, kwa hiyo hata operesheni ya dawa za kulevya,” amesema.

“Tukifanya kazi kwa pamoja tuna uwezo wa kujikuta habari za dawa kwenye mkoa wetu zinakuwa historia na huwezi kukuta biashara hii ina nguvu kama hakuna rushwa na hasa kwenye mpaka wetu wa Namanga dawa zinapenya,” ameongeza Makonda.

“Sasa biashara hii ina watu wengi wanaonufaika nayo, haiwezi kuwa vita ya mtu mmoja. Kama mimi nitapambana na dawa peke yangu siwezi, lazima tufanye kama timu, eneo la rushwa linabeba mambo mengi,” ameongeza.

Ametolea mfano katika Kituo cha Polisi Muriet, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha alifanya mabadiliko katika kituo hicho kilikuwa kinalalamikiwa kutokana na baadhi ya askari kutokuwa waadilifu.

“Nilitamani mwezi wa saba kabla hatujaenda kufanya operesheni mitaani, tuanze ndani yetu. Kama kuna mtu uhamiaji anatuchafua tutoe taarifa sisi wote tunataka hela lakini si hela hii tutapoteza heshima yetu, tusafishane ili tuwapate watu ambao ni waadilifu,” amesema.

“Kuna kipindi TRA wakiomba msaada wa kwenda kukamata watu wanaokwepa kodi na kutengeneza bidhaa feki, kuna wengine hawapewi taarifa mapema inabidi waviziane wapeane taarifa siku ya tukio kwani wakipeana mapema habari imeharibika.”

“Sasa kwa nini ifike hatua hiyo, taasisi nyingine inashindwa kuwapa taarifa mapema, kwa hiyo ni tamanio langu kwamba tuweke mkakati kwetu ndani yetu kwa kusaidiana, nataka tutengeneze familia moja,” ameongeza.

Kuimarisha usalama
Kuhusu mafuta amesema amepata mdau ambaye amejitolea mafuta na yatakuwa yakitolewa kwa taasisi hizo za ulinzi na usalama ambapo kila taasisi inapata kulingana na uhitaji wake.

Amesema kati ya lita 20,000, lita 10,000 ni petroli na lita 10,000 ni dizeli ambapo Jeshi la Polisi litakuwa likipata lita 12,000, Uhamiaji lita 2,000, Zimamoto lita 1,000, Magereza lita 1,000, JWTZ lita 1,000.

“Ili kuongeza utendaji kazi na kuwe na nguvu ya utendaji tunataka Jeshi la Polisi litupe matokeo mazuri, habari ya tatu mzuka Arusha iwe historia, wazazi ambao mnafahamu watoto wetu wana hiyo tabia imefika wakati kila abiria achunge mzigo wake, tutaendesha operesheni tusije kulaumiana, tunataka kutokomeza uhalifu,” amesema.

“Alikuja mdau kunitembelea akaniuliza nataka anisapoti kwenye nini, nikamwambia mafuta ili vyombo vya ulinzi na usalama viwe na mafuta, mwananchi akihitaji huduma akapiga simu msiwe na kigezo mafuta yameisha,” amesema.

Makonda amesema mafuta hayo yatakuwa endelevu ili kuimarisha doria, ulinzi na kutoa huduma haraka kwa wananchi ikiwemo pale wanapohitaji Zimamoto au Polisi.

Katika hatua nyingine, Makonda amewataka watendaji hao kushirikiana na waandishi wa habari ili wasije kuripoti taarifa zisizo sahihi.

Akizungumzia hilo, Kamanda wa Polisi Arusha, Justine Masejo, amewataka waandishi wa habari kuwa wazalendo katika nchi yao.

“Arusha tuna viwili ambavyo ni utalii na kilimo cha mbogamboga, sisi kwa nafasi zetu kila mmoja na mchango wake katika hayo. Niombe waandishi wa habari kuwa wazalendo na siyo kupaka nchi matope na msishindwe kusema maovu tunayoyafanya, mtukosoe pia,” amesema.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema mapambano ya rushwa ni dhana shirikishi na kama kuna vihatarishi vya usalama wa nchi rushwa ni mojawapo, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema Takukuru ilifanya utafiti mdogo na kubaini migogoro mingi ya ardhi inafikishwa katika ngazi za juu kwa sababu ngazi za chini kwenye mabaraza hakuna uwezeshwaji, hivyo yanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kwenye halmashauri ukusanyaji wa kodi kuna aina fulani ya udhaifu wa kimfumo ila naamini tukishirikiana tutapata suluhu ya pamoja,” amesema.

Related Posts