Beki mpya JKT aota makubwa

BEKI mpya wa JKT Tanzania, Abdulrahim Seif Bausi aliyesajiliwa kutoka Uhamiaji ya Zanzibar, amesema anatambua Ligi Kuu Bara ni ngumu na inahitaji utulivu na kujituma, ili aweze kung’ara msimu ujao.

Beki huyo ni mtoto wa kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Seif Bausi, alisema alikuwa anaifuatilia ligi ya Bara, hivyo haoni kama itampa changamoto kubwa.

“Jambo la msingi ni kujituma katika mazoezi ili kupambania kupata nafasi, mengine ni ya kawaida,” alisema Bausi ambaye nje na soka ni Afisa uhamiaji, kazi ambayo hakuwa tayari kuifafanua zaidi.

Alisema beki ambaye alikuwa anamfuatilia zaidi ligi ya Bara ni  Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ wa Yanga, aliyemuelezea msimu ulioisha alifanya vizuri.

“Bacca ni mshikaji wangu, ndio maana ilikuwa rahisi sana Yanga ikicheza kumfuatilia, amefanya kazi kubwa na kiwango chake kilikuwa muhimu ndani ya klabu yake, kitu ambacho nimejifunza kwake ni nidhamu na bidii,” alisema Bausi Jr na kuongeza;

“Hakuna kitu kinachoweza kushindikana ukijituma na kujifunza kwa wengine ambao wanafanya vizuri, lakini jambo la muhimu kwangu kwa sasa nina furaha kuichezea JKT Tanzania, nashukuru viongozi kwa kuniamini niwe sehemu ya kikosi chao.”

Related Posts