Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, amewaagiza wataalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi waliopo kwenye maonyesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki kuandaa taarifa ya tathmini ya maonyesho hayo ili kubaini jinsi yalivyowanufaisha wakulima wadogo, hususan katika kuongeza tija ya uzalishaji.
Kunenge ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Agosti 5, 2024 baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya wakulima Nanenane katika kanda hiyo.
Amesisitiza pamoja na kuandaa taarifa hiyo ya tathmini, wataalamu hao wanapaswa pia kuandaa taarifa itakayobainisha namna maonyesho hayo yatakavyosaidia kutekeleza ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Tanzania kulisha Afrika na Dunia.
“Maofisa ugani, Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pikipiki kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wenu, lazima mjiulize hizo pikipiki zinasaidiaje kuongeza tija kwa wakulima. Watembeleeni wakulima, wafugaji na wavuvi. Kanda yetu inapaswa kuwa tofauti na nyingine katika uzalishaji.
“Tufanye vitu kwa kuacha alama na tuwasaidie wakulima wetu, wafugaji wetu na wavuvi wetu. Rais Samia ameleta mbolea ya ruzuku, teknolojia za kisasa zipo na mbegu bora zipo,” amesema.
Kunenge pia amewataka wataalamu hao kuacha kufanya tathmini kwa kuangalia idadi ya wakulima waliofika kwenye mabanda ya maonyesho hayo, bali wafanye tathmini kwa kuzingatia jinsi teknolojia zilizopo zimewasaidia wakulima kuongeza tija.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya ‘Farm Base’ inayotengeneza viuatilifu, mbolea na dawa mbalimbali za kilimo na uvuvi, Suleiman Msellem amesema katika maonyesho ya mwaka huu wamekuja na teknolojia mpya ya dawa ya kuua mchwa shambani na nyumbani inayotengenezwa kwa maganda ya korosho.
Msellemu ameeleza kuwa dawa hiyo inaitwa “DKO”, imefanyiwa utafiti na kuthibitika kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na mchwa, ambao ni waharibifu wa mazao na pia huleta usumbufu nyumbani na maeneo mengine ya makazi.
Ameongeza kuwa teknolojia hiyo imesaidia kuongeza thamani ya zao la korosho linalolimwa, hasa katika ukanda wa mikoa ya mashariki, kwani awali maganda ya korosho yalikuwa yakionekana hayana thamani na kutupwa, lakini sasa yanatumika kutengeneza dawa hiyo.
Faida za dawa hiyo, mbali na kuangamiza mchwa, pia haina kemikali yoyote ya ziada, hivyo ni rafiki kwa mazingira na salama kwa matumizi.
Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima nchini (Mviwata), Steven Luvuga amesema mtandao huo umekuwa ukiwafundisha wakulima kufanya kilimo hai kisichotumia mbolea na dawa zenye kemikali.
Pia Mviwata imekuwa ikihimiza wakulima kutumia mbegu, dawa na mbolea za asili, ili kuepuka utegemezi wa pembejeo za dukani.