Mwili wa Mchungaji Kantate kuagwa leo, mazishi Old Moshi

Hai. Mwili wa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kimashuku, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Kantate Munis (42) aliyefariki dunia kwa ajali ya gari utaagwa leo Alhamisi, Agosti 8, 2024 katika Kanisa la Ebenezer alilokuwa akihudumu.

Mbali na Kantate, mwingine aliyefariki  dunia kwenye ajali hiyo iliyotokea Jumapili Agosti 4, 2024  eneo la Kimashuku,  Kata ya Mnadani Wilaya ya Hai, ni mzee wake wa usharika, Laban Kweka (50).

Ajali hiyo ilitokea  wakati mchungaji huyo akikata kona kutoka barabarani kwenda upande wa kulia ili kuingia kanisani kwake na ndipo aligongwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi  iliyotolewa na usharika huo leo Alhamisi, Agosti 8, 2024 mwili huo utaagwa kuanzia saa 4:50 asubuhi mpaka saa 6:50 mchana ikiwa ni pamoja na kutoa salamu za rambirambi.

Ratiba hiyo inaeleza, baaada ya kumalizika kwa salamu za rambirambi kutafanyika ibada ya kuaga mwili usharikani hapo kuanzia saa 7:00 hadi saa 9:00 mchana na kisha mwili wa mchungaji huyo utaondoka kwa msafara kuelekea Kijijini Kisamo Old Moshi, Wilaya ya Moshi kwa ajili ya taratibu za maziko ambayo yatafanyika kesho Ijumaa Agosti 9, 2024.

Mchungaji Kantante pamoja na Mzee wake wa Ushirika, Laban Kweka (50) ambaye anazikwa leo Agosti 8, 2024 walifariki dunia  kwa ajali Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiri wakitokea kwenye uimbaji usharika wa Gezaulole wilayani Hai, kugongwa na basi kubwa la abiria  wakati akikata kona kuingia usharika wa Kimashuku ambako anaishi.

Hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amenukuliwa akisema dereva wa basi lililosababisha ajali hiyo amekamatwa kwa taratibu za kisheria kwa kuwa alifanya uzembe kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

Mchungaji Kantate ameacha mume na watoto watoto wanne.