Wazazi watakiwa kuimarisha uhusiano na watoto wao

Dar es Salaam. Wazazi wametakiwa kuimarisha uhusiano na watoto wao kwa kuwauliza maswali ya maana ili kuelewa hisia na mawazo yao.

Imeelezwa kuwa, njia hiyo itasaidia kulinda misingi ya imani na kuzuia matatizo ya baadaye yawakumbayo vijana.

Haya yamesemwa leo Jumapili Agosti 11, 2024 katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Masheikh na Kizazi cha Kuleta Mageuzi, lililoandaliwa na Islamic Foundation.

Sheikh Wasim Kempson kutoka Uingereza akizungumza katika kongamano hilo, amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na watoto wao.

Amesema lengo ni kuwasaidia kujua na kukabiliana na changamoto za maisha zikiwamo za mmomonyoko wa maadili huku akionya kuhusu hatari za tamaa na vishawishi vinavyoenezwa na teknolojia na mitandao ya kijamii.

“Wazazi ingizeni upendo wa Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (SAW) katika nyoyo na akili za watoto. Hii ni njia muhimu ya kuhakikisha wanakua na misingi imara ya kiimani itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha,”amesema Kempson.

Amesema nyakati zilizopita, watu wenye ujuzi walikuwa wengi huku wahubiri wakiwa wachache lakini siku zijazo, wahubiri wataongezeka lakini wenye ujuzi na maarifa watapungua.

Naye Sheikh Shahid Muhammad kutoka Tanzania, ameelezea umuhimu wa wazazi kuwafundisha watoto wao misingi ya dini na maadili kama ilivyoelekezwa na Mtume Muhammad (SAW), akionya kuhusu uvamizi katika dini na uhaba wa walimu wenye maarifa.

Hivyo, amewataka wazazi kuwafundisha watoto historia ya dini na kuwakataza kutenda mambo yasiyofaa na wajiepushe na tamaduni zinazokwenda kinyume na maelekezo ya vitabu vya Mungu.

Sheikh Assim Al-Hakeem kutoka Saudia, ameelezea umuhimu wa wanandoa kuheshimiana na kutegemeana, huku akisisitiza majukumu ya wanawake katika ndoa yana umuhimu mkubwa.

“Majukumu muhimu ambayo wanawake wanayo katika ndoa, kama vile kutunza nyumba na kusaidia waume zao na kujitolea kwa wanawake katika majukumu haya kunaweza kuwapeleka kwenye Jannah (Pepo),” amesema Sheikh Al-Hakeem.

Katika Kongamano hilo, kijana Abdulkarim Omary kutoka Chuo cha Morogoro Islamic, ametoa wito kwa vijana kuzingatia maadili na ushirikiano katika kuunda jamii bora huku akisema kuwa kila kizazi kina jukumu la kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii.

“Kila kizazi kina jukumu la kuhakikisha, kinachangia kwenye maendeleo na ustawi wa jamii kwa kuzingatia maadili mema na ushirikiano,” amesema Abdulkarim.

Related Posts