10 Kali za mwanzo kwa Pamba, KenGold

RATIBA ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, imewekwa hadharani, huku tukishuhudia timu mbili zilizokuwa zinacheza Ligi ya Championship za Pamba ya Mwanza na KenGold ya Mbeya zikipishana na Mtibwa Sugar na Geita Gold zilizoshuka rasmi daraja.

Wakati mashabiki wa timu hizo za Pamba na KenGold wakiwa na mzuka na kusubiria kile ambacho miamba hiyo itakifanya kwa msimu huu, Mwanaspoti linakuletea  michezo 10 ya mwanzoni kwa kila timu na zinapaswa kujipanga ipasavyo.

Timu hii ya jijini Mwanza, imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Ligi ya Championship msimu uliopita kufuatia kushinda michezo 20 kati ya 30, sare saba na kupoteza mitatu na kujikusanyia jumla ya pointi 67.

Pamba imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kusota kwa takribani miaka 23, tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, huku msimu huu ikiwa imejiimarisha vizuri kwa kushusha wachezaji bora na benchi la ufundi linaloongozwa na Mserbia, Goran Kopunovic.

Kikosi hiki naanza kufungua pazia la Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza leo Agosti 16 dhidi ya Tanzania Prisons, kisha kushuka uwanjani hapo katika mchezo wake wa pili wa msimu kwa kupambana na Dodoma Jiji Agosti 24.

Timu hiyo itaendelea kusalia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kwa kuzikaribisha Singida Black Stars Septemba 15 kisha ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’ Mashujaa Septemba 21 na kuanza safari ya ugenini dhidi ya Coastal Union, Mkwakwani Tanga Septemba 28.

Baada ya hapo itaanza safari ya kuja jijini Dar es Salaam kwa michezo miwili ikianza na mabingwa watetezi Yanga Oktoba 3 na Oktoba 21, kucheza na Azam FC, kisha kurejea CCM Kirumba kupambana na Kagera Sugar, Oktoba 24, mzunguko wa nane.

Raundi ya tisa ya timu hiyo, itakuwa ugenini kucheza na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi Oktoba 25 ingawa huenda ratiba ikabadilishwa kwani Oktoba 24 inacheza na Kagera Sugar, kisha kuifuata Tabora United, Ali Hassan Mwinyi Novemba 2.

KenGold iliyosota katika Ligi ya Championship kwa misimu mitatu mfululizo, imejihakikishia nafasi ya Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kutwaa ubingwa huo baada ya kumaliza kinara ikiwa na jumla ya pointi 70, katika michezo 30, iliyocheza.

Timu hiyo ya Chunya Mbeya, ilijihakikishia ubingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita baada ya kushinda michezo 21, sare saba na kupoteza miwili tu kati ya 30, ikifunga jumla ya mabao 51 na kuruhusu 18 na kujikusanyia pointi zake 70.

KenGold itaanza kumenyana na Singida Black Stars Agosti 18, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya na kucheza michezo mitatu mfululizo ugenini ikianza na Fountain Gate Septemba 11, Uwanja wa Tanzanite, KMC Septemba 16 kisha Kagera Sugar Septemba 20.

Baada ya hapo, itarejea katika Uwanja wa Sokoine Mbeya kucheza michezo mitatu mfululizo ukianza wa Septemba 25, dhidi ya mabingwa watetezi msimu uliopita Yanga, Tabora United Septemba 28, kisha kupambana na Maafande wa JKT Tanzania Oktoba 4.

Oktoba 26, itakuwa Lake Tanganyika Kigoma kucheza na Mashujaa na baada ya hapo itatua jijini Dar es Salaam kucheza na Azam FC, mechi ambayo itapangiwa tarehe kisha kuhitimisha mzunguko wa 10, Mbeya kwa kupambana na Dodoma Jiji Novemba 2.

Akizungumzia ratiba ya michezo hiyo, Kocha Mkuu wa Pamba Mserbia, Goran Kopunovic anasema, hana mashaka na maandalizi na usajili wa nyota wapya ambao kikosi hicho imefanya huku jambo kubwa akiomba sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Mwanza.

“Sio rahisi kwa sababu ukiangalia ratiba ilivyokuwa tunaanza na timu nzuri ambazo ni wazoefu na Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu sasa, tumefanya maandalizi kwa kiwango kikubwa, hivyo tuko tayari kushindana pia na kila aliyekuwa mbele yetu.”

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa KenGold, Fikiri Elias anasema, licha ya timu hiyo kutopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu, ila mashabiki na wadau mbalimbali wa soka watashangazwa na kile watakachokiona wakati msimu utakapoanza.

“Usajili tuliofanya hauzungumzwi sana kwa sababu ni wachezaji ambao wanaonekana wa kawaida machoni mwa watu, niseme tu wazi, tumehakikisha kwanza tunabaki na nyota walioipambania timu hii na baada ya hapo tukaongeza wachache wenye uwezo.”