KWA SASA kinachoendelea kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kule mitandaoni ni ishu ya ujio wa straika mpya wa Simba yakitajwa majina mawili, Christian Leonel Ateba anayekipiga USM Alger na Elvis Kamsoba aliyemaliza mkataba na Perserikatan Sepakbola ya Indonesia.
Simba ilianza msimu vibaya kwa kuondoshwa kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya mtani wake Yanga kwa bao 1-0 la Maxi Nzengeli kabla ya wananchi hao kwenda kubeba kombe hilo mbele ya Azam FC kwa kuichapa mabao 4-1 katika mechi ya fainali.
Baada ya mechi ya nusu fainali kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids alihojiwa na vyombo vya habari na kudai kuwa hajaridhishwa na viwango vya washambuliaji wake.
Washambuliaji hao ni Steven Mukwala ambaye ndio ilikuwa mechi yake ya kwanza ya dabi tangu alipojiunga na wanamsimbazi hao akitokea Asante Kotoko ya Ghana.
Wengine ni Kibu Denis, Fredy Michael ambao tayari wamecheza ligi na Valentino Mashaka aliyejiunga na Simba katika dirisha hili akitokea Geita Gold FC.
Wachezaji hao kwenye mechi mbili za ngao hawakufunga dhidi ya Yanga na Coastal Union na kumfanya kocha huyo aagiziwe fasta straika mpya.
Fadlu aliyetangazwa kuinoa Simba Julai 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha, ameweka wazi kutoridhishwa na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, hivyo kuwataka mabosi wa kikosi hicho kuanza mchakato huo haraka.
Bado ni mapema sana kujua ubora wa baadhi ya wachezaji wa Simba hasa eneo la ushambuliaji ingawa timu kubwa haziangalii muda.
Simba iliweka kambi nchini Misri na kucheza baadhi ya mechi za kirafiki, swali ni kwamba je, kocha hakuona kama kuna udhaifu eneo la ushambuliaji hadi kwenye mechi moja tu ya dabi.
Kinachotokea kwa Simba kwenye kipindi hiki cha usajili ni presha ya mechi mbili tu za Ngao ya Jamii ambazo kwa haraka haraka zigo lote linamwangukia Mukwala kutokana na nafasi alizozipata na kushindwa kuzitumia.
Ukweli ni kwamba si kila mchezaji anaweza kuingia kwenye mfumo wa kocha moja kwa moja mfano mzuri Joseph Guede ambaye alipojiunga na Yanga dirisha dogo karibu kila shabiki aliona ni straika mbaya lakini baada ya muda alizoea na kuonesha kiwango bora.
Kinachotokea kwa Mukwala si kwamba ni mshambuliaji mbaya bali bado hajazoea mazingira ya Tanzania pamoja na wenzake.
Presha kubwa ambayo kwa sasa Simba inapitia ni kutokana na muendelezo wa ubora wa watani wao Yanga hususani kwenye usajili.
Msimu huu Yanga imeongeza wachezaji saba Duke Abuya, Shadrack Boka, Clatous Chama, Aziz Andambwile, Khomeiny Aboubakar, Prince Dube na Jean Baleke.
Hadi sasa tayari wachezaji sita wamecheza na kuwafanya Yanga watambe baada ya kuonyesha kiwango bora kuanzia kwa viungo na washambuliaji.
Mastraika wapya wa Yanga, Dube na Baleke tayari wamefunga kwenye mechi walizopewa jambo linaloifanya Simba itafakari inakwama wapi.
Lakini ukiangalia kuna utofauti kidogo kwa mastraika wa Yanga wote wawili wamecheza ligi ya Tanzania na wanaifahamu vyema jambo lililowapa urahisi ilihali Simba ni wageni.