Dar es Salaam. Jitihada za mwenyekiti wa zamani wa Halmashauri ya Mkuranga mkoani Pwani, Juma Abeid, kujinasua na adhabu ya kulipa faini ya Sh700,000 au kifungo cha miaka 4, zimekwaa kisiki katika Mahakama ya Rufani nchini Tanzania.
Mwaka 2021, Abeid alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh440,000 kutoka kwa Bashiru Chande ili aitumie kufanikisha mchakato wa kumhamisha mkewe kutoka Babati hadi Mkuranga.
Mkewe huyo, Husna Tegera, aliyekuwa shahidi wa saba wa Jamhuri alikuwa ni mwajiriwa wa Serikali akiwa mwalimu katika Halmashauri ya Babati Mkoa wa Manyara, ambapo Abeid alitumiwa fedha hizo kupitia simu yake ya mkononi.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh700,000 au kutumikia kifungo cha miaka 4 jela, endapo angeshindwa kulipa faini.
Hakuridhishwa na hukumu hiyo na akakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, ingawa hata hivyo Jaji Emmanel Ngigwana aliyeisikiliza rufaa hiyo aliitupa, akieleza upande wa mashitaka ulithibitisha shitaka hilo.
Hakuridhishwa na hukumu hiyo na kukata tena rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania ambayo nayo katika hukumu yake iliyoitoa Agosti 15,2024 ilifuta mwenendo mzima wa kesi ya rufaa katika Mahakama Kuu kutokana na dosari za kisheria.
Baada ya kufuta mwenendo huo, Jopo la majaji watatu, Ferdnand Wambali, Lilian Mashaka na Benhaji Masoud walimtaka Abeid kukata upya rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, kama bado ana nia ya kuendelea kupinga kutiwa kwake hatiani.
Kosa la rushwa lilivyokuwa
Katika kosa lililomtia hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo, ilielezwa kuwa kati ya Januari 1,2019 na Julai 22,2019 akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Abeid alijipatia fedha hizo kwa njia ya rushwa kutoka kwa Chande.
Ilielezwa kuwa alijipatia kiasi hicho cha fedha baada ya kuhamishiwa kupitia simu yake na Chande ambapo katika usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashitaka uliita mashahidi wanane kuthibitisha shitaka, akiwamo Chande na mkewe, Husna.
Fedha hizo zilitumwa kupitia kwa wakala aitwaye Pauline Mgunda aliyekuwa shahidi wa tatu wa Jamhuri na kwamba mwenyekiti alimtambulisha Chande aliyekuwa shahidi wa pili kwa Ofisa Elimu wa Mkuranga aliyekuwa shahidi wa kwanza.
Katika ushahidi huo, shahidi wa sita, Paulina Masampala akiwa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Babati, alieleza kuwa aliwahi kupigiwa simu na mtu ambaye hamfahamu akimwelezea kuhusu suala la kumuhamisha Husna.
Hata hivyo, alisema hakuweza kusaidia kumuhamisha mwalimu huyo kwa sababu hapo Babati kulikuwa na walimu wachache wa sayansi katika shule nyingi za sekondari, hivyo isingekuwa busara kumuhamisha mwalimu huyo kutoka Babati.
Shahidi wa nane, Beneth Kapinga ambaye ni Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Mkuranga alisema kupitia upelelezi wao, alikuwa na maoni kuwa mwenyekiti huyo alikuwa amejihusisha na vitendo vya rushwa.
Katika utetezi wake, Abeid alikanusha vikali tuhuma hizo na kuita mashahidi watatu kumtetea, lakini baada ya usikilizaji kukamilika, mahakama ilimtia hatiani na kumuhukumu kulipa faini ya Sh700,000 na akishindwa atumikie kifungo jela.
Hakuridhika na hukumu hiyo na akakata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam ambayo ilitupiliwa mbali na Jaji Ngigwana, lakini bado hakuridhika ndipo akakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambako nako amekwaa kisiki.
Katika usikilizwaji wa rufaa yake Mahakama ya Rufani mwenyekiti huyo wa zamani wa Halmashauri aliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Daniel Ngudungi huku Jamhuri ikitetewa na mawakili wa Serikali, Fidesta Uisso na Clarence Mosha.
Hata hivyo katika hoja zake za kuunga mkono rufaa hiyo, wakili Ngudungi alikubaliana na hoja ya kisheria iliyoibuliwa na wakili Uiso kuhusiana dosari za kisheria zilizobainika katika mwenendo wa rufaa yake Mahakama Kuu.
Alieleza kuwa ingawa hakumwakilisha mrufani Mahakama Kuu, lakini alipopitia jalada halisi na kumbukumbu za rufaa mbele ya mahakama hiyo, amebaini hapakuwepo notisi ya kukata rufaa iliyokuwa imewasilishwa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, hiyo ni kwenda kinyume na takwa la kifungu namba 361(1)(a) ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA), na kukiri kuwa kukosekana kwa notisi hiyo, kunafanya mahakama isikilize rufaa isiyo sawa.
Kutokana na hilo, aliiomba mahakama itamke kuwa mwenendo wa rufaa katika Mahakama Kuu ulikuwa batili na hivyo mahakama ibatilishe mwenendo huo.
Hata hivyo, mbali na kuomba jopo la majaji libatilishe mwenendo huo, aliwasihi waendelee kusikiliza rufaa ya mteja wake kwa kurejea upya mwenendo huo, kwa kuegemea sababu zao za rufaa hasa hoja ya upendeleo wa Hakimu Mkuranga.
Wakili Uisso kwa upande wake, aliungana na wakili Ngudungi kuiomba mahakama ibatilishe mwenendo wa kesi ya rufaa Mahakama Kuu katika rufaa namba 41 ya 2021, na kusisitiza hapakuwepo notisi ya rufaa iliyowasilishwa ndani ya siku 10.
Hata hivyo, hakukubaliana na hoja ya wakili Ngudungi ya kutaka Mahakama ya Rufani iendelee kusikiliza rufaa na baadaye kurejea mwenendo huo, badala yake aliiomba mahakama kubatilisha mwenendo wote wa kesi Mahakama Kuu.
Wakili Uisso alienda mbali na kueleza kuwa kama mrufani bado anataka kuendelea kupigania haki yake kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, basi afanye mchakato huo kwa mujibu wa sheria za rufaa zilizopo.
Katika hukumu yao, walisema wamepitia kwa umakini mwenendo wa kesi ya rufaa Mahakama Kuu na wanakubaliana kuwa rufaa ya mrufani mbele ya hiyo ilikuwa batili kutokana na kukosekana kwa notisi ya kukata rufaa.
Majaji hao walisema kilichopo katika mwenendo huo ni sababu za rufaa ambazo huwa zinawasilishwa ndani ya siku 45 tangu kutolewa kwa hukumu na adhabu, lakini sheria inataka lazima kuwepo notisi ya maandishi ya nia ya kukata rufaa.
Walisema kwa masikitiko, Mahakama Kuu ilipitiwa na takwa hilo la kisheria la kutaka uwepo wa notisi ya kukata rufaa na kusema mahakama husikiliza rufaa pale ambapo inakuwa iko sahihi (competent) kulingana na sheria za nchi.
Majaji hao walikataa hoja ya wakili wa mrufani kwamba licha ya mwenendo wa kile kinachoitwa rufaa katika mahakama kuu kufutwa, itumie mamlaka yake kusikiliza na kuamua kuhusiana na malalamiko dhidi ya mahakama ya Mkuranga.
Kwa mujibu wa majaji, baada ya kubatilisha mwenendo huo, ni hiari ya mrufani kukata rufaa upya Mahakama Kuu kupinga hukumu ya mahakama ya Wilaya ya Mkuranga kwa kufuata sheria zinazoongoza mchakato wa kukata rufaa.