SIKU chache baada ya uongozi wa Mtibwa Sugar kumrejesha aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Swabri Aboubakar baada ya kikosi hicho kushuka daraja, bosi huyo ameanza kupiga hesabu kali kwa nia ya kurejesha heshima ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara 1999 na 2000.
Swabri aliondolewa kikosini humo Desemba 29, mwaka jana nafasi yake ikichukuliwa na Abdulrahman Joshi ingawa baada ya timu hiyo kushuka daraja kutokana na mwenendo mbaya wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, viongozi wameamua kumrejesha tena.
Akizungumza na Mwanaspoti, Swabri alithibitisha kurejea katika nafasi hiyo, huku akiomba sapoti ya wadau mbalimbali wa soka wa mkoani Morogoro kuendelea kukisapoti kikosi hicho, ili kitimize malengo ya kurudi katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
“Sio rahisi kupandisha timu kwenda Ligi Kuu Bara hivyo tunahitaji kushikamana sasa kwa sababu ni kazi yetu sote, naamini uwezo huo tunao ikiwa tutashirikiana kuanzia mwanzo hadi mwishoni ili tutimize malengo ambayo tumejiwekea,” alisema.
Baada ya kurejea kwa Swabri tayari timu hiyo imefanya maboresho ya kikosi chao ambacho kitashiriki Ligi ya Championship msimu huu, huku kikimtangaza aliyekuwa kocha wa Gwambina FC, Coastal Union na Dodoma Jiji, Melis Medo, raia wa Marekani.
Pia Mtibwa imefanya maboresho kwa kuwaongeza baadhi ya nyota wapya wakiwemo aliyekuwa kipa wa Geita Gold, Costantine Malimi, mabeki wa kati, Erick Kyaruzi na Aman Kyata na washambuliaji, George Makang’a, Anuary Jabir na Raizin Hafidh.