LONDON, ENGLAND: LINAPOKUJA suala la kuishinda Manchester City kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya miamba hiyo ya Etihad kubeba mara nne mfululizo, Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anaamini timu yake safari itakuwa makini kutimiza ndoto za kumaliza ukame wa taji hilo.
Alipoulizwa kuhusu mpango wake wa msimu huu, kocha huyo Mhispaniola alisema atapambana kwa kadri ya uwezo wake kushinda pointi nyingi zaidi kuliko timu nyingine zote, alisema: “Tunatafuta pointi 114. Kama tukifanya hivyo, tutashinda ubingwa wa ligi hakika, huo ndiyo mpango.”
Ni dhahiri, Arteta alikuwa anatania. Hakuna timu iliyowahi kushinda mechi zote 38 kwenye msimu wa Ligi Kuu England.
Na zaidi, timu moja tu ndiyo iliyowahi kufikisha pointi 100. Hiyo ilikuwa kwenye msimu wa 2017/18, wakati Man City iliposhinda mechi 32, sare nne na vichapo viwili na kubeba ubingwa kwa tofauti ya pointi 19.
Pointi nyingi zaidi ambazo timu ilipata na kisha haikushinda ubingwa, ilikuwa pointi 97, zilizovunwa na Liverpool kwa msimu wa 2018/19, ambao walimaliza kwenye nafasi ya pili.
Pointi nyingi za bingwa wa Ligi Kuu England
Timu Msimu Pointi Nafasi
Man City 2017/18 100 1
Liverpool 2019/20 99 1
Man City 2018/19 98 1
Liverpool 2018/19 97 2
Chelsea 2004/05 95 1
Kwa rekodi hizo, inaonyesha pointi chini ya 100 zitatosha kupata ubingwa msimu huu. Lakini, ni chini kiasi gani? Je, timu inahitaji nini?
Kwa takwimu za misimu 32 iliyopita kwenye Ligi Kuu England, ikiwamo mitatu ya mwanzo, wakati klabu zilipocheza mechi 42 kila moja kwa msimu.
Ni mara mbili tu timu ilibeba ubingwa kwa kukusanya pointi chini ya 80 – na ilikuwa Manchester United katika msimu wa 1996/97 na 1998/99 – kwa kipindi hiki, pointi hizo hazitoshi tena kunyakua ubingwa.
Kwa wastani wa ubingwa kwenye Ligi Kuu England ni pointi 87.8. Lakini, kwa rekodi za hivi karibuni, wastani huo wa pointi 87.8 haziwezi kutoa bingwa kwa msimu wa 2024/25 na hiyo ni kwa sababu ya mtu mmoja tu, Pep Guardiola.
Tangu msimu wa 2016/17, wakati Guardiola alipotua kwenye ligi, wastani wa pointi za ubingwa kwa sasa ni 93.6, lakini ikishuka kidogo kwa misimu miwili iliyopita na kuwa na wastani wa 90.0.
Je, ni pointi kiasi gani kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England? Guardiola atakuwa kwenye kibarua kizito cha kufanya hilo, wakati atakapoliongoza chama lake la Man City kushinda ubingwa wa tano mfululizo.
Nani ataizuia Man City kubeba ubingwa wa tano mfululizo? Kinachoelezwa ni Liverpool na Arsenal zinaweza kupambana na Man City kwenye mbio za ubingwa wa msimu wa 2024-25. Liverpool, ambayo ilibeba ubingwa mmoja tu msimu wa 2018/19 ilifanya hivyo mbele ya makali ya Man City na kwa misimu sita iliyopita, miamba hiyo ya Anfield ina wastani wa pointi 84.3.
Pointi za Liverpool kwa misimu sita iliyopita
Msimu Pointi Nafasi
2018/19 97 2
2019/20 99 1
2020/21 69 3
2021/22 92 2
2022/23 67 5
2023/24 82 3
Aston Villa ilimaliza nafasi ya nne msimu uliopita, pointi 23 nyuma na mabingwa Man City, hivyo kocha wa miamba hiya Villa Park, Unai Emery anafahamu wazi timu yake inapaswa kucheza kwa kiwango cha aina gani ili kufanikiwa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England.
“Ni ndoto kushinda ubingwa. Lakini, ni ngumu sana,” alisema Emery. “Wakati tulipoanza msimu wa 2023/24, tulipocheza mechi mbili dhidi ya Man City na Arsenal na kushinda zote, tulijiona tupo kwenye nafasi hiyo ya ubingwa.
“Lakini, zile timu nyingine zenyewe zina mwendelezo mzuri wa matokeo chanya. Nataka kufanya vizuti zaidi na ndoto zangu siku zote nimekuwa nikiziamini. Ni wazi mpango wangu mkubwa ni kushinda taji la Ligi Kuu England au Ligi ya Mabingwa Ulaya.”