TOTAL FOOTBALL: Nani atatoboa? | Mwanaspoti

MANCHESTER, ENGLAND: KUELEKEA msimu huu wa Ligi Kuu England mmoja kati ya mastaa wanaotarajiwa kufanya makubwa ni straika wa Manchester City, Erling Haaland.

Haaland ambaye alijiunga na Man City mwaka 2022, anatarajiwa kuvunja rekodi mbalimbali zinazoendelea kuishi katika ligi hiyo.

Moja kati ya rekodi hizo ni ile ya Dixie Dean aliyefunga mabao 60 ya EPL msimu wa 1927-28 akiwa na Everton ambayo imeendelea kuishi hadi leo.

Huyo ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi ya EPL ndani ya msimu mmoja na Haaland alihitaji mabao 24 kwa msimu uliopita ili kufikia idadi hiyo.

Pia Haaland ana kazi nyingine ya kuvunja rekodi iliyoachwa na Dean ya kuwa mchezaji wa timu ya England aliyefunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja, Dean alitupia mabao 63 ya michuano yote katika msimu 1927/28.

Katika msimu wake wa kwanza Haaland alikuwa karibu kuifikia rekodi hiyo baada ya kufunga mabao 52 ya michuano yote akiwa na Man City.

Watu wengi waliamini angevunja rekodi hiyo kwani alikuwa amebakisha mechi 10 wakati amefunga mabao 50, lakini alishindwa kufanikisha na katika mechi hizo za mwisho alifunga mabao mawili tu.

Mbali ya deni la Dean, Haaland pia ana deni kwa Lionel Messi la kuwa mchezaji aliyeifungia timu yake mabao mengi ndani ya msimu mmoja. Messi aliifungia Barcelona mabao 73 msimu wa 2011-12.

Staa huyu wa kimataifa wa Norway pia msimu huu anasubiriwa na rekodi zilizopo Man City, kwa sasa yeye ndio mchezaji anayeshikilia rekodi ya kuifungia Man City mabao mengi ndani ya msimu mmoja akiivunja rekodi ya miaka 94 ya Tommy Johnson ndani ya msimu wake wa kwanza alipotupia kambani mara 52.

Msimu huu anaweza kuingia katika orodha ya wafungaji bora 20 wa muda wote wa timu hiyo.

Katika Ligi ya Mabingwa nako anasubiriwa kwa hamu. Hadi sasa Haaland amefunga mabao 35 katika mechi 30 za Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kumfanya kuwa katika nafasi ya 21 katika orodha ya wafungaji wa mashindano hayo.

Amechukua tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo mara mbili hali inayofanya kuwa mmoja kati ya wachezaji waliobuka wafungaji bora mara nyingi zaidi katika historia ya Uefa akizidiwa na wachezaji saba walio juu yake.

Ikiwa atafanikiwa kuwa mfungaji bora na msimu huu, wachezaji pekee watakaomzidi katika rekodi hiyo ni Cristiano Ronaldo, Messi na gwiji wa Bayern Munich, Gerd Muller.

Haaland pia anaweza kuvunja rekodi ya Ronaldo ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa alipofanya hivyo msimu wa 2013/14 katika mechi 11.

Related Posts