Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi ameeleza kukerwa na kitendo cha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kutelekeza jengo la bweni lililogharimu zaidi ya Sh78 milioni bila kulikamilisha kwa takriban miaka saba.
Jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2017 katika Shule ya Sekondari Ngoreme wilayani Serengeti kwa nguvu za wananchi pamoja na wanafunzi waliowahi kusoma Sh18 milioni.
Kufuatia hali hiyo, Mtambi ametoa wiki sita kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha jengo hilo ambalo linatarajiwa kutumiwa na wanafunzi 80 wa kike.
Mtambi ametoa maagizo hayo Agosti 17, 2024 baada ya kutembelea shule hiyo ambapo pamoja na mambo mengine imebainishwa kuwa ukosefu wa bweni ni moja ya changamoto zinazokabili shule hiyo.
“Haiwezekani jiwe la msingi limewekwa na mbio za mwenge mwaka 2017 lakini hadi sasa jengo halijakamilika, wananchi wamejitolea hadi kufikia hapa halmashauri inashindwa nini kukamilisha hili jengo. Mnataka mzigo wote ubebwe na wananchi, hii haikubaliki, mkurugenzi nakupa wiki sita jengo hili liwe limekamilika,” amesema Mtambi.
Amesema inasikitisha kuona miradi mingi ya maendeleo ya jamii ikitekelezwa na wahisani pamoja na nguvu za wananchi na kuhoji ni namna gani halmashauri hiyo inatumia fedha zake za mapato ya ndani.
“Tumepita hapa na mbio za mwenge, miradi yote inayofanyika ni ufadhili ni ufadhili, ni ufadhili nyie halmashauri fedha mnazokusanya mnafanyia nini?” amehoji.
Amesema jengo hilo ambalo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 80 linahitaji takriban Sh30 milioni ili liweze kukamilika na kuanza kutumika, gharama ambazo amesema halmashauri hiyo inamudu hasa ikizingatiwa sehemu kubwa ya gharama za ujenzi imetolewa na wananchi.
Mkuu wa shule hiyo, Daniel Edward amesema kutokana na kukosa bweni, wamelazimika kutumia madarasa kwa ajili ya wanafunzi kulala wakati utaratibu mwingine ukiendelea.
“Tulikuwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, mwaka huu tumepangiwa wengine 92 wa kidato cha tano ambao kati yao 73 wamekwisharipoti. Kutokana na changamoto hii imebidi tutumie madarasa kama njia mbadala wakati tukisubiri utaratibu mwingine kwa sababu pesa za ujenzi wa mabweni na miundombinu mingine zimetolewa na Serikali lakini zimekuja kwa kuchelewa,” amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma amesema jengo hilo limechelewa kukamilika kutokana na halmashauri hiyo kutokuwa na fedha kwa wakati huo.
“Unajua miradi hii ya nguvu za wananchi mara nyingi inategemea sapoti ya Serikali, sasa ikitokea fedha hakuna kwa kipindi hicho basi kila kitu kinakwama na kushindwa kufikia malengo.
“Tumepitia wakati mgumu hapo nyuma, kulikuwa na Uviko-19, hivyo nguvu ya halmashauri kidogo ilipungua, ila tayari jambo linashughulikiwa kwani hapakuwa na shida nyingine zaidi,” ameongeza Makuruma.
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wazazi wa wanafunzi shuleni hapo, wamesema wamesikitishwa na kitendo cha halmashauri yao kushindwa kukamilisha jengo hilo na kupelekea wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.
“Serikali imeshindwa kuwaunga mkono wananchi, hili jengo ni kama limekamilika maana vitu vilivyobakia ni vichache sana lakini badala yake limetelekezwa hapo wakati kuna uhitaji wa bweni shuleni,” amesema Msamba Makenge.
Ghati Moremi amesema hali hiyo inawakatisha tamaa wananchi kujitolea nguvu zao kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hivyo ni vema ukawepo utaratibu wa Serikali kuunga mkono jitihada zao.