Matatizo Ya Mikataba Ya Wachezaji

MWAKA 2000, Yanga ilimsajili kijana wa kidato cha pili shule ya sekondari Makongo, aliyekuwa akiichezea Kagera Stars (sasa Kagera Sugar), aliyeitwa Ephraim Makoye.

Baadaye ikabainika kuwa kijana huyo pia alisajiliwa na Simba, hivyo kuzua utata mkubwa.

Wakati huo mambo ya mikataba ya wachezaji na klabu hayakuwapo na wala chama cha soka (FAT) hakikuyatambua kabisa.

Kilichofanyika ni chama chenyewe (FAT) kutoa fomu za usajili na klabu kuzichukua na kuandika majina ya wachezaji wao watakaokuwa nao siku husika.

Halafu FAT itakaa na kuyapitia hayo majina na kutoa taarifa ya uthibitisho. Wachezaji waliopitishwa wanaandikwa ‘CLEARED’, ambao hawakupitishwa wanaandikwa ‘NOT CLEARED’, usajili unafungwa.

Jina la Ephraim Makoye lilionekana kwenye fomu za Yanga na Simba, hivyo akawa NOT CLEARED.

Kesi ikanguruma na fomu za usajili zilipoangaliwa, ikaonekana ya Yanga ilitangulia kwenda, hivyo Simba wakaonekana wakorofi.

Simba wao wakapeleka mkataba waliosaini na mchezaji huyo ambao ulikuwa na tarehe ya nyuma kuliko hata fomu za usajili za Yanga.

Lakini FAT wakaukataa mkataba kuutumia kama kielelezo kwa sababu wakati huo mikataba ilikuwa haitambuliwi.

Kama klabu itasaini mkataba na mchezaji utabaki kuwa wa kwao, lakini FAT haiutambui, na hautumiki kwenye usajili.

FAT ikaamuru Makoye aende Yanga kwa sababu ndiyo waliotangulia kumsajili, japo hawakuwa na mkataba naye.

Simba waliokuwa na mkataba naye, wakamkosa.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha kabla ya mikataba kuanza kutumika hapa nchini.

Wakati wa usajili, wachezaji walikuwa wanajisajili kwenye timu zaidi ya moja.

Kwa mfano, mwaka 1980, nyota wa Taifa Stars, Mtemi Ramadhan aliyekuwa akiichezea timu ya Waziri Mkuu SC ya Dodoma, alisajiliwa na timu nne.

Waziri Mkuu SC, Pan Africa SC, Simba SC na Yanga SC.

Mchezaji huyu alisajiliwa na timu hizi zote kabla ya Taifa Stars kwenda Nigeria kwenye fainali za AFCON.

Siku wanarudi, viongozi wa timu zote hizo nne wakafika uwanja wa ndege kumpokea, wakajikuta wakichapana makonde na kuzua tafrani kubwa sana.

Lakini sasa TFF ambaye ni mrithi wa FAT, anaitambua mikataba kutokana na miongozo ya FIFA.

Tatizo la wachezaji kusajiliwa na timu zaidi ya moja limepungua sana, ila limeibuka tatizo jipya la wachezaji kutoiheshimu mikataba yao waliyosaini wao wenyewe.

Mchezaji anasaini mkataba yeye mwenyewe halafu anaukana, kama ilivyotokea kwa wachezaji kadhaa.

Mizozo ya wachezaji na klabu juu ya mikataba yao au tafsiri ya vipengele kwenye mikataba imekuwa mingi sana.

Kwa mfano mzozo wa Feisal Salum na klabu yake ya Yanga au mzozo wa Prince Dube na klabu yake ya Azam.

Upande mmoja wa mkataba, yaani mchezaji, unaamua tu kuachana na upande mwingine, yaani klabu, bila kufuata vipengele…au unafuata lakini upande wa pili hautaki.

Kupitia makala hii, nitachambua kwa kina namna pande mbili za mikataba zinavyoweza kuepuka migongano katika kuachana kwao, kwa kutumia migano rahisi na halisi.

Kuna njia tatu pekee zinazoruhusu mkataba wa mchezaji kufikia ukomo kabla ya muda wake, yaani kuvunjika; damage, release clause na buy out clause.

Kama lilivyo neno damage yaani uharibifu, njia hii husababishwa na uharibifu wa mkataba yaani ukiukwaji wa vipengele uliofanywa na upande mmoja.

Kwa jina jingine njia hii huitwa UNILATERAL TERMINATION yaani upande mmoja kuvunja mkataba.

Ili njia hii itumike, ni lazima upande mmoja uwe na sababu ya msingi, (JUST CAUSE) ikiwamo ukiukwaji wa vipengele kama malipo au sababu za msingi za kimichezo kama kutopata nafasi.

Upande unaovunja mkataba hautakiwi kulipa chochote.

Hii ndiyo njia ambayo Saimon Msuva aliitumia kuvunja mkataba wake na Wydad Casablanca.

Pia Manchester United iliitumia kuvunja mkataba na Cristiano Ronaldo.

Ronaldo alibakisha miaka miwili kwenye mkataba wake na Manchester United, lakini alipoenda kufanya mahojiano na Piers Morgan akiichamba klabu, akawa amekiuka vipengele na hiyo ikawa JUST CAUSE, yaani sababu ya msingi.

Manchester United ikatumia sababu hiyo ya msingi kuvunja mkataba bila kumlipa. Bila hivyo wangetakiwa wamlipe matrilioni ya pesa.

Release ni neno la Kiingereza ambalo kwa Kiswahili maana yake ni kuondosha yaani kufanya kitu kiondoke au kitoke…au kuachilia.

Clause maana yake ni kipengele.

Kwa hiyo Release Clause maana yake ni kipengele cha kuondosha au kuachilia.

Kwenye mikataba ya wachezaji, kipengele hiki kipo kwa ajili ya kuipa nafasi klabu kumuachia mchezaji aondoke endapo kuna klabu nyingine imeleta ofa sahihi.

Mara nyingi kipengele hiki huendana na masharti mengine kwa mfano timu husika kushuka daraja au kufuzu mashindano makubwa nk.

Kwa mfano klabu A ina mkataba na mchezaji XY, wenye kipengele kinachosema endapo klabu hiyo itashuka daraja basi mchezaji husika ataruhusiwa kujiunga na klabu nyingine ya daraja la juu kwa kiasi fulani kwa ada ya shilingi kadhaa.

Kwa hiyo klabu hiyo ikishuka daraja, halafu ikaja klabu nyingine ikiwa na kiasi kilichotajwa, basi ile klabu lazima imuuze huyo mchezaji.

Mfano sahihi wa kipengele hiki upo kwenye kesi ya mwaka 2013 ya Luis Suarez na klabu yake ya Liverpool.

Mkataba wake ulikuwa na kipengele kama hiki kilichosema klabu yake itaweza kumuuza kwa ada ya zaidi ya Pauni 40 milioni kwenda timu itakayofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, endapo Liverpool haitafuzu.

Na kweli, mwaka ule Liverpool haikufuzu, Arsenal ambao walifuzu wakataka kutumia hicho kipengele.

Walipoona ada ya zaidi ya Pauni 40 milioni, basi wakatoa milioni 40 halafu wakaongeza pauni moja kama moja yaani ukiiandika kwa tarakimu ofa yao ilikuwa ni Pauni 40,000,001.

Liverpool wakakataa, wakisema kambi ya Suarez haikuutafsiri vizuri mkataba ule na mmiliki wa Liverpool akawashangaa Arsenal kwa kuongeza pauni moja, akauliza ‘hivi hawa Arsenal huwa wanavuta nini pale Emirates’?

Kumbe kile kipengele kilisema endapo timu itakuja na ada ya zaidi ya Pauni 40 milioni, inaweza kuanza mazungumzo na Liverpool, lakini ikitaka kumchukua moja kwa moja hata bila mazungumzo, ilitakiwa itoe zaidi ya Pauni 45 milioni.

Arsenal ikamkosa Suarez, kwa kutokuwa na taarifa sahihi za RELEASE CLAUSE.

Na hivi pia ndivyo alivyofanya Valentino Mashaka wa Geita Gold.

Mkataba wake ulikuwa na kipengele cha kushuka daraja, iliposhuka akaenda Simba.

Buy out maana yake ni kununua yaani kumlipa mtu hela ili aachie umiliki wa kitu chake.

Clause maana yake ni kipengele.

Kwa hiyo ‘buy out clause’ maana yake ni kipengele cha kununua.

Hiki ni kipengele kinachotoa nafasi kwa mchezaji kuununua mkataba wake ili awe huru.

Kipengele hiki lazima kiseme mchezaji akitaka kuondoka alipe fedha kiasi kadhaa.

Yaani badala ya klabu fulani kuja kumnunua, mchezaji mwenyewe anaununua mkataba wake na anakuwa huru.

Hivi ndivyo alivyofanya Neymar alipoondoka Barcelona mwaka 2017.

Mkataba wake ulikuwa na kipengele hili chenye thamani ya Euro milioni 222.

Akachukua pesa, akaweka kwenye akaunti…akasepa.

Hii haihitaji mazungumzo wala sababu ya msingi, unachotakiwa kuwa nacho ni pesa tu.

Related Posts