TRA kutumia Ndondo Cup kutoa elimu ya kodi

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikilenga kutanua wigo wa walipa kodi ili kuongeza mapato yanayokusanywa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuja na mkakati ili kufikia watu wengi zaidi na kuwapatia elimu ya kodi na ulipaji kodi kihalali.

Ili kufanikisha hili TRA imejipanga kutumia mashindano ya Ndondo Cup kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu Stempu za Kielektroniki za Ushuru (ETS) na kampeni ya Hakiki Stampu.

Hilo litafanyika kupitia udhamini wa Sh40.5 milioni iliyotoa na kuifanya kuwa mdhamini wa mashindano hayo. Udhamini huu unaashiria dhamira ya TRA ya kukuza ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya kodi kupitia michezo huku ikikuza mipango muhimu ya elimu ya kodi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema ujumbe muhimu wa udhamini huo ni kuangazia umuhimu wa kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kuhakikisha kuwa ni salama, ni halisi na zinatii kanuni za kodi.

“Ushirikiano huu na Ndondo Cup ni fursa ya kipekee kwa TRA kuwasiliana na wananchi kwa njia sahihi. Kupitia michezo, tunaweza kufikia hadhira kubwa zaidi ili kuwaelimisha na kuwashawishi kufahamu suluhisho la kisasa zaidi la Stempu za Ushuru za Kielektroniki katika kuhakikisha uhalisi wa bidhaa,” amesema Kayombo.

Amesema wanaamini kupitia mpango huo wanaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa tabia za watumiaji na kuchangia katika lengo pana la kuimarisha uzingatiaji wa kodi kote nchini.

“TRA inatoa wito kwa watumiaji wa bidhaa zenye Stempu za Ushuru za Kielektroniki (ETS) kupakua programu ya Uthibitishaji wa Stempu na kuhakiki bidhaa hizo kabla ya kuzitumia. Hii ni njia mojawapo ya kulinda afya zao na kuhakikisha serikali inapata mapato sahihi ya kodi,” amesema Kayombo.

Udhamini huo unaosimamiwa na kampuni ya Shadaka Sports Management, utasaidia michuano ya Ndondo Cup inayoendelea ambayo ni miongoni mwa mashindano maarufu ya soka nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Usimamizi wa Michezo wa Shadaka, Shaffih Dauda aliishukuru TRA huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa makampuni katika kuongeza thamani ya michezo ya ndani.

‘Tunafuraha kuwa na TRA kama wadhamini wakuu wa Ndondo Cup mwaka huu. Udhamini huu sio tu kwamba unasaidia maendeleo ya soka la chini lakini pia una lengo kubwa zaidi kwa kuelimisha umma juu ya masuala muhimu ya kodi, vilevile viwanja vyetu vya michezo vinajaa bidhaa mbalimbali, hivyo tunatarajia ushirikiano huu ili kuhakikisha teknolojia hii inasaidia. tujikinge na bidhaa feki kwa tunapokuwa viwanjani,” amesema Dauda.

Ndondo Cup imekuwa ikiadhimishwa kwa muda mrefu kwa namna inavyokuza vipaji vya soka vya ndani na kuleta jamii pamoja.

Kwa msaada wa TRA, mashindano ya mwaka huu yanapangwa sio tu kuburudisha bali pia kuelimisha umma kuhusu masuala muhimu yanayohusiana na kodi, kuhimizia umuhimu wa kufuata sheria na manufaa ya mfumo wa Stampu za Kielektroniki za Ushuru na Hakiki Stempu

Related Posts