Sumbawanga. Wakili wa kujitegemea, Deogratius Sanga, ametumia mistari ya Biblia, kama moja ya sababu za kuiomba mahakama iwape adhabu ndogo watuhumiwa wawili, waliokiri kosa la kumuua Ignas Bonventure bila kukusudia.
Mbele ya Jaji, wakili alitumia Mstari wa Luka 17:4 unaosema; “Na kama akikukosa mara saba katika siku moja na kurudi kwako mara saba akisema nimetubu, msamehe,” kuwaombea washtakiwa wa mauaji, Ladslaus Richard (54) na Raymond Kizila (62).
Ilielezwa mahakamani kuwa Novemba 23, 2021 katika eneo la Matanga Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, washtakiwa hao walisababisha kifo cha Ignas Bonventure waliyemkamata usiku wa manane wakati wakifanya doria.
Kulingana na maelezo ya kosa hilo, Bonventure alishukiwa kuwa mwizi na maelezo yake ya kwa nini anatembea mitaani usiku wa manane hayakuaminika na matokeo yake, kundi la watu waliokuwepo usiku huo waliamua kumwadhibu kwa kipigo.
Katika kumpiga huko, Bonventure alipata majeraha na alifariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi ndani na nje ya mwili wake kwa mujibu wa uchunguzi wa mwili uliofanywa na Dk Elina Yesaha.
Inaelezwa washtakiwa walikamatwa siku hiyohiyo na wengine waliokuwepo hawakukamatwa na baada ya upelelezi kukamilika, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) iliwafungulia mashtaka ya kuua kwa makusudi kinyume na kifungu 196.
Hata hivyo, waliposomewa mashtaka yao Agosti 19, 2024 mbele ya Jaji Thadeo Mwenempazi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, washtakiwa hao waliomba kukiri kosa dogo la kuua bila kukusudia, ombi ambalo lilikubaliwa.
Maombi ya mawakili mbele ya Jaji
Kabla ya kutamka adhabu, upande wa mashtaka uliomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa wakiitaka izingatie kwamba kuna uhai wa mtu umepotea na wakosaji hawakutumia nguvu ya kiasi, kushughulika na marehemu.
Jaji Mwenempazi alisema ni maoni ya upande wa mashtaka kuwa wakosaji hao na washirika wao walipaswa kutafuta ukweli juu ya kile alichokisema marehemu walipomkamata usiku ule wa manane, badala ya kuamua kumpiga.
Kwa upande wake, wakili aliyekuwa akiwatetea washtakiwa aliiomba mahakama iwape adhabu ndogo kwa kuwa kosa hilo ni la kwanza na wamekiri,pia hata wao wamejikuta kwenye shida kutokana na watu wenye hasira kuamua kutekeleza kipigo hicho kilichosababisha kifo.
Wakili Sanga alisema wateja wake hao walijikuta kwenye matatizo wakati wanafanya doria kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao, na walikuwa katika ‘misheni’ ya kuhakikisha jamii ya eneo hilo inakuwa salama.
“Ni bahati mbaya kuwa kitendo kilichofanywa na watu wenye hasira kimewafanya wawe hapo walipo leo. Washtakiwa wote ni wazee wana umri wa miaka 54 na 62 mtawalia na wanasumbuliwa na maradhi kutokana na uzee,”alisema wakili na kuongeza;
“Washitakiwa wako mahabusu kwa miaka miwili na miezi tisa sasa na katika kipindi hicho walichokaa mahabusu wamejifunza na wanajutia na ndio maana leo (Agosti 19, 2024) wameamua kukiri kosa hili.”
Wakili huyo wa utetezi aliomba adhabu ndogo na msamaha akinukuu kitabu cha kilichomo ndani ya Biblia Takatifu, Luka mstari wa 17:4 kwamba katika kutoa adhabu, mahakama iwape kifungo cha nje badala ya cha gerezani.
Alichokisema Jaji katika adhabu
Baada ya mawasilisho ya mawakili wa pande zote mbili, Jaji alisema anachukua taarifa kuwa washtakiwa hao wamejikuta katika mgogoro huo wa sheria wakiwa katika wajibu wa kuhakikisha amani inakuwepo katika eneo wanaloishi.
“Ninaamini, kama sio wananchi wenye hasira kali, labda uamuzi katika eneo la tukio ungekuwa tofauti na kile kilichotokea. Ninafahamu walikuwa wengi na katika kundi kubwa lakini waliotambuliwa kuwepo ni washtakiwa.”
“Kwa upande mmoja, usalama wa watu na mali zao ni muhimu na ni jambo la kupongezwa na kutia moyo kwa wananchi kushiriki kikamilifu,”alieleza Jaji.
Hata hivyo, Jaji alisema wale wanaoshiriki katika ulinzi shirikishi lazima wafahamu kuwa hata wanaowashuku kuwa ni hatari, lazima wapelekwe katika vyombo vya kisheria ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa msingi huo, Jaji Mwenempazi alisema ana maoni kuwa muda ambao washtakiwa wameutumikia mahabusu ni funzo kwao, hivyo anawaachia huru kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai katika kipindi cha miezi 12.