Njombe. Mkazi wa Kijiji cha Ugabwa kilichopo wilayani Makete Mkoa wa Njombe, Sarah Chaula (17) amelazimika kuacha masomo ili awatunze wadogo zake wawili alioachiwa na wazazi wake walioondoka nyumbani kwa nyakati na sababu tofauti.
Awali baba wa familia ndiye anayedaiwa kutangulia kuondoka nyumbani hapo baada ya kutofautiana na mama wa familia hiyo, baadaye mama naye aliondoka kwa madai ya kukimbia kulipa deni la Sh2 milioni linalodaiwa kusababishwa na mtoto wake wa kiume, ambaye naye haijulikani alipo.
Chaula ameyasema hayo leo Jumapili Agosti 25, 2024 alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital kijijini kwao Ugabwa.
Amesema alikuwa miongoni mwa wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka 2022 katika Shule ya Sekondari Ilumaki iliyopo wilayani Makete Mkoa wa Njombe na mwaka huu alipaswa kuwa kidato cha tatu.
Amesema kwa sasa ameshindwa kuendelea na masomo kwa kile alichoeleza ni kuzidiwa na jukumu la malezi ya wadogo zake wawili wanaosoma shule ya msingi.
Amesema amelazimika kubeba jukumu hilo aliloachiwa na wazazi wake ambao hajui mpaka sasa wametimkia wapi.
“Yaani niseme kiufupi maisha ni magumu sana kwangu, sijazoea maana kila kitu nilikuwa nategemea kwa mama yangu ambaye sasa hayupo, nimegeuka mzazi wa wadogo zangu, wale, wavae waende shule, japokuwa napenda sana kusoma, lakini ndiyo hivyo,” amesema Chaula.
Amesema mbali na mgogoro (bila kuutaja ni wa nini) wa baba na mama uliomfanya baba kuondoka nyumbani, lakini deni la Sh2 milioni lililosababishwa na kaka yake likawafanya kaka yake huyo sambamba na mama yake waondoke nyumbani na kumtelekezea wadogo zake.
Chaula amesema anaishi kwa kufanya vibarua vya kulima, kupalilia na kuvuna mazao mashambani ili apate ujira utakaomwezesha kupata fedha za kujikimu yeye na wadogo zake.
Chaula amesema hivi sasa taratibu ndoto yake ya kuendelea na elimu ya sekondari inapotea na badala yake anatamani kupata elimu ya ufundi, ili apate ujuzi utakaomsaidia kujikimu kimaisha.
“Kama nitapata shule za ufundi itanisaidia kwa sababu nikiangalia nyuma nina wadogo zangu ambao wananifuata wanatakiwa kwenda shule” amesema Chaula.
Wadogo zake ambao Nuru Chaula anayejiandaa na mtihani wa darasa la saba mwaka huu (13) huku Faraja Chaula akiwa darasa la nne (10) ambao wote wanasoma Shule ya Msingi Ugabwa wamesema wanamshukuru dada yao ila wanatamani wangeendelea kufurahia uwepo wa mama yao.
“Dada anatusaidia kupata mboga, chumvi, sukari na hela za kusagia mahindi ili tupate unga wa ugali na mama angekuwepo angetusaidia kutulea, kutuchunga na kutujali,” amesema mdogo wake Chaula.
Kauli ya mwenyekiti wa kitongoji
Mwenyekiti wa kitongoji cha Wang’ele kilichopo kijiji cha Ugabwa, Eden Mahenge amesema msichana huyo amebeba majukumu mazito ambayo hakutakiwa kuwa nayo bali yalipaswa kuwa ya wazazi wake.
Mmoja wa majirani zake Chaula aliyejitambulisha kwa jina la Getrude Ngole amesema licha ya msaada mwingine anaoutoa kwenye familia hiyo, mchango mwingine ni kuendelea kumsihi awe makini kwa sababu mazingira aliyopo hivi sasa ni hatarishi.
“Huyu ni binti kuna wengine wanajua ni mke wa kuoa, lakini ukweli ni mtoto na yupo peke yake kwa hiyo ni mazingira hatarishi kwake,” amesema Ngole.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilumaki ambako alikuwa akisoma Sarah, Christom Mturo amesema ni vema msichana huyo akasaidiwa kupata elimu ya ufundi ambayo anahitaji kwa sababu tayari ameamua kuachana na elimu ya sekondari.
Amesema mara nyingi migogoro ya familia imekuwa ikichangia kuharibu ndoto za watoto kutokana na wazazi kutengana na kuwaacha peke yao wakihangaika.