RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza wachezaji wa gofu wa kike wa Tanzania kwa kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya nchi nje ya mipaka yake huku akiahidi kuleta kocha wa kigeni kwa ajili ya kuifundisha timu ya Taifa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Damas Ndumbaro kufuatia mchezaji nyota wa Tanzania, Madina Idd kushinda taji la mashindano ya wazi ya wanawake ya Uganda, (Uganda Ladies Open Championships) yaliyomalizika Jumamosi jioni mjini Entebbe.
Madina hakuanza vizuri katika mashindano hayo, alishinda akitokea nyuma na kukusanya jumla ya mikwaju 228 na kumpita Mtanzania mwenzake, Hawa Wanyeche aliyemaliza wa pili kwa mikwaju 230 na Mganda, Martha Babirye aliyepata mikwaju 232 katika nafasi ya tatu sawa na Mtanzania, Neema Olomi aliyepata idadi hiyo hiyo ya mikwaju.
Mbali ya ushindi huo, Mtanzania Aaalaa Riyaz Somji aliweka historia kwa kupiga mpira na kuingia moja kwa moja kwenye shimo namba sita ambalo jumla ya mikwaju mitatu inatakiwa kupigwa mpaka mpira kuingia kwenye shimo.
Ndumbaro alisema, Rais Samia amefurahishwa sana na matokeo mazuri ya wachezaji wa gofu wanawake na kuamua kuleta kocha ambaye atalipwa mshahara na serikali.
“Nimeongea na Rais Samia na amewapongeza Madina Idd na wenzake kwa matokeo mazuri na kushinda kwenye mashindano ya gofu ya wanawake nchini Uganda, ni fahari kwa Tanzania,” alisema Waziri Ndumbaro.
Alisema watawasiliana na uongozi wa Chama cha Gofu cha Wanawake ili kufanikisha hilo kwani anaamini kuwa, Tanzania ina wachezaji nyota zaidi ambao wanaweza kufanya vyema nje ya mipaka yake.
“Madina na wenzake wameiperusha vyema bendera ya nchi na wanastahili pongezi kubwa sana, tunaamini, watafanya vyema katika mashindano mengine ya yanayokuja, ” alisema.
Aliongeza kuwa wanataka kuwa na wachezaji ambao wataiwezesha Tanzania kuendelea kung’ara na kwa sasa serikali imeandaa mtaala wa mchezo wa gofu ambao utafundishwa katika chuo cha michezo cha Malya.
“Tunaandaa uwanja wa gofu wa mashino 9 chuo cha Malya ambao utatumika kufundishia walimu wa gofu kwa ajili ya shule ya msingi na sekondari..tunataka michezo ijayo ya Umiseta na Umitashumta kuwe na michezo ya gofu, lengo ni kuundeleza mchezo huu,” alisema.