COASTAL Union ya Tanga imerudia kile kile ilichowahi kukifanya mwaka 1989 ilipong’olewa raundi za awali za michuano ya CAF, baada ya jioni ya leo kutoka suluhu na AS Bravo ya Angola na kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0.
Coastal ilipoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 3-0 na leo ilikuwa ikihitaji ushindi wa zaidi ya mabao matatu, lakini ikaishia kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na kuungana na Azam FC, JKU na Uhamiaji zilizoaga mapema michuano hiyo ya CAF kwa msimu huu.
Katika mchezo huo Coastal ilipoteza penalti ya dakika za mapema baada ya Mkenya, John Mark Makwata kushindwa kukwamia mkwaju wake wavuni kutokana na kosa la beki mmoja wa Bravo kuunawa mpira katika harakati za kuokoa mpira.
Wagosi walipata nafasi ya kucheza michuano hiyo baada ya kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara iliyopita, ikiwa ni mara ya pili baada ya kucheza mara ya kwanza michuano ya CAF mwaka 1989 katika Kombe la Washindi ambao mwaka 2004 liliungwanishwa na Kombe la CAF kuwa michuano hiyo ya sasa.
Katika michuano hiyo ya mwaka 1989 ilitolewa na Costa do Sol ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 5-2, ikifungwa nyumbani mabao 3-2 na kupigwa 2-0 ugenini na tangu hapo haikuwahi kushiriki michuano hiyo hadi ilipoingia mwaka huu kwa nchi ya Tanzania kuwakilishwa na timu mbili kwa kila shindano la CAF.
Yanga iliyofuzu kwa kishindo katika Ligi ya Mabingwa kwa kuing’oa Vital’O ya Burundi pamoja na Simba iliyoanzia raundi ya pili kikitarajiwa kuvaana na Al Ahli Tripoli ya Libya iliyoitoa Uhamiaji ya Zanzibar ndizo timu pekee za Tanzania zilizosalia katika michuano hiyo kati ya timu sita zilizoshiriki msimu huu.
Azam iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo mwaka 2004 baada ya awali kuicheza 2015, ilipata aibu kwa kung’olewa na APR kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya jana usiku kufungwa mabao 2-0 jijini Kigali baada ya awali kushinda nyumbani Chamazi kwa bao 1-0.
JKU ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) ilikumbana na kipigo cha jumla ya mabao 9-1 mbele ya Pyramids ya Misri ambao sasa itavaana na APR, wakati Uhamiaji iling’oka kwa jumla ya mabao 5-1 kwa Al Ahly Tripoli ikifungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza na juzi Ijumaa kulala tena 3-1.
Msimu uliopita Yanga na Simba ndizo zilizotinga makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na zikavuka hadi robo fainali na kung’olewa na vigogo Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga iliyotinga hatua hiyo baada ya miaka 25 iling’olewa kwa penalti na Mamelodi baada ya kutoka suluhu nyumbani na ugenini wakati Simba ilicharazwa nje ndani kwa jumla ya mabao 3-0. Ahly ilitetea taji hilo mbele ya Esperance wa Tunisia.