MATOKEO ya sare mfululizo katika michezo miwili yameonekana kuwatibua Tanzania Prisons, huku wakiahidi kusahihisha makosa ili mechi zinazofuata wafanye kweli.
Prisons imeanzia ugenini Ligi Kuu ikicheza mechi mbili dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa na haijaonja ushindi wowote wala bao la kuotea na kujikita nafasi ya nne kwa pointi mbili.
Maafande hao wataendelea kubaki ugenini kwa mchezo wa tatu mfululizo watakapoifuata Tabora United, Septemba 14 kabla ya kuwakaribisha Simba, Oktoba 22 mwaka huu.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Renatus Shija alisema licha ya kutopata ushindi katika mechi hizo, lakini pointi mbili za ugenini siyo matokeo mabaya japokuwa hesabu zao ilikuwa ni kuvuna pointi sita.
Alisema kwa sasa benchi la ufundi linaenda kujipanga upya kusahihisha makosa hasa eneo la ushambuliaji kuhakikisha nafasi wanazopata wanazitumia vyema kupata mabao.
“Tulikuwa na matarajio ya kushinda michezo yote lakini haikuwa bahati, vijana walipambana ila wapinzani nao wakaonesha ushindani tukaambulia pointi mbili.”
“Tulitengeneza nafasi nyingi katika michezo yote japokuwa haikuwa bahati yetu kufunga mabao, tunaenda kusahihisha makosa ili mechi zinazofuata tuweze kupata ushindi,” alisema Shija.
Kocha huyo alisema Prisons itafanya vizuri kwani benchi la ufundi limeona mwenendo wa kikosi hicho kutokuwa mbaya kutokana na jinsi wachezaji wanavyocheza uwanjani.