Bodaboda zinavyoacha simanzi anguko la kiuchumi

Dar es Salaam. “Tangu mume wangu amefariki dunia, maisha yamekuwa magumu, mimi na Watoto wangu kula yetu Mungu ndiye anajua maana hatuna uhakika wa kesho yetu itakavyokua.”

Ndivyo alivyoanza kusimulia Leticia Justine (si jina halisi) ambaye ni mama wa watoto wawili ambaye mume wake alifariki dunia mwaka 2020 kwa ajali ya kugongwa na gari akiwa katika majukumu yake ya kila siku kama dereva bodaboda.

Wakati mumewe anafariki dunia, binti yake wa kwanza alikuwa na miaka mitatu huku Leticia akiwa na mimba ya miezi minne ya mwanaye wa pili wa kiume.

Mumewe alipofariki dunia, Leticia hakuwa na biashara yoyote anayofanya kutokana na hali ya ujauzito aliyokuwa nayo, hii ilitokana na kuwa na homa mara kwa mara na kuacha kazi ya kuuza duka la dawa alikokuwa ameajiriwa.

 “Mume wangu alipofariki nilijua nimeumbuka, ndiye alikuwa kila kitu. Mtoto alikuwa anasoma shule nzuri ya kulipia sasa hivi hata haeleweki,” anasema Leticia.

Anasema walikuwa wameanza kuinukia kwani mumewe alikuwa amejenga nyumba ambapo mpaka anafariki ilikuwa imeezekwa vyumba viwili.  “Sasa ni zaidi ya miaka mitatu, hakuna kilichobadilika, angekuwepo mume wangu tungekuwa tumefika mbali, nawaza angekuwa hajajenga hata hiki kibanda sijui tungekuwa tunaishi maisha gani na hawa watoto wangu, tumegeuka ombaomba kwa ndugu na wategemezi,” anasema.

Mbali na Leticia aliyeachiwa familia, kwa Peter John (39) ni tofauti. John ambaye ni dereva bodaboda, alipata ajali eneo la Buguruni mataa na kuvunjika mguu wa kushoto wakati akimkwepa mwenda kwa miguu.

Ajali hiyo ilitokea Mei 3, 2024, Peter anasema aliyumba wakati anamkwepa mtembea kwa miguu baada ya taa kuruhusu, jambo lililomfanya kuanguka na gari lililokuwa nyuma yake lilimkanyaga mguu wake na akapelekwa Hospitali ya Amana kwa matibabu.

Kwa mujibu wa Peter, familia yake kwa sasa inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

“Familia yote inanitegemea katika kila kitu na sasa nipo chini siwezi kufanya jambo lolote litakaloleta pesa nyumbani na kuna wakati inanibidi nitoe hadi akiba yangu,” anasema Peter baba wa watoto wanne akiwamo aliyemaliza kidato cha nne.

“Sasa hivi natoa fedha tu, siingizi kama zamani, imefika hatua inabidi niombe msaada kwa baadhi ya ndugu, kitendo ambacho sikukizoea, nawapa mzigo watu ambao hawakuwa na mategemeo nao,” anasema.

Akizungumzia hali ya nyumba kwa sasa, Subira mke wake Peter anasema mumewe alikuwa anategemewa na familia yao.

“Ajali hii imekuwa pigo kubwa kwa familia hasa ikizingatiwa tuna watoto wanne pia baba yangu alikuja hapa nyumbani kwa ajili ya matibabu. Lakini sasa amekaa tu hapati huduma ya hospitali kwa sababu mume wangu tuliyekuwa tukimtegemea hatoki tena kutafuta pesa kama zamani,”anasema Subira, maarufu mama wawili.

Pia, amesema wamejikuta wakiingia gharama kubwa ya kumtibu Peter kwa sababu hana bima ya afya, hivyo kutakiwa kutoa fedha taslimu na mpaka sasa wameshatoa zaidi ya Sh200,000 na bado wanatakiwa kurudi tena hospitali.

Kuhusu gharama alizozungumzia Subira, Serikali pia imekuwa ikizisema kuwa ajali hizo zinaongeza mzigo kwenye  mfumo wa huduma za afya nchini na sehemu kubwa ya bajeti hutumika kwa matibabu ya majeruhi wa ajali za pikipiki.

Wawili hawa wanawakilisha kundi kubwa la watu ambao wamepoteza ndugu zao kwa ajali za bodaboda na baadhi wakipata ulemavu wa kudumu jambo linalobadili maisha yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani 2023, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023 jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio ya ajali 448 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 13 sawa na asilimia 2.9. Hata hivyo, katika kipindi hicho, idadi ya vifo vya ajali za barabarani iliongezeka kwa vifo 44 kutoka vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022 hadi vifo 376 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 13.3.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani, ajali hizi husababishwa na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na kutofuata sheria za usalama barabarani.

“Uchakavu wa vyombo vya usafiri, ubovu wa miundombinu, ulevi, uzembe, uwepo wa vipuri visivyokidhi viwango pia ni sababu ya kuwapo kwa ajali hizi,” imeeleza ripoti ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, hali hii inaweza kuwa zaidi ya inavyoripotiwa kwa sababu Taasisi ya Tiba na Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), imesema inapokea takribani majeruhi wa ajali za barabarani 700 kwa mwezi.

Kati ya majeruhi hao, asilimia 60 ambayo ni sawa na majeruhi sita kati ya 10 wanatokana na ajali zinazohusiana na pikipiki maarufu bodaboda.

Takwimu hizo zilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa MOI, Dk Lemeri Mchome Jumanne ya Julai 2, 2024 hospitalini hapo, wakati akipokea msaada wa fedha pamoja na viti mwendo kutoka kampuni ya Watu Credit.

“Kwa kiwango kikubwa wagonjwa wengi wana uhusiano wa moja kwa moja na ajali za pikipiki aidha walikuwa abiria, dereva wa bajaji au gari limepata ajali kwa sababu lilikuwa linakwepa bodaboda au bajaji,” alisema Dk Mchome.

Alisema asilimia 75 ya majeruhi hao hawana ndugu na hawana msaada wa kifedha kugharamia matibabu kwa kuwa ajali zikitokea wanaletwa na raia wema pamoja na askari wa usalama barabarani.

“Asilimia 25 iliyobakia ni vijana ambao hawana ndugu kabisa, walikuja mjini kutafuta kipato. Tunakaa nao kwa zaidi ya miezi mitatu, gharama zinaongezeka,” alieleza Dk Mchome. 

Pia amesema wengi wao wanaumia vichwani, huku asilimia 75 wanaumia mikono na miguu:

Hivyo, anasema kutokana na Sera ya Afya, Wizara inawagharamia matibabu, lakini baadaye ndugu wakijitokeza wanaombwa kuchangia matibabu hayo.

Kutokana na kutambua sababu hizo, Jeshi la Polisi idara ya usalama barabarani limeeleza mikakati yake katika kudhibiti ajali hizo,  ambapo miongoni mwake ni kudhibiti mwendo kasi kwa kuweka vituo vya ukaguzi wa ratiba za magari ya abiria.

“Kuimarisha doria na ukaguzi barabarani, kutoa adhabu stahiki kwa wakosaji, kusimamia utaratibu wa kuondoa pointi za sifa za udereva kwa kila kosa na hatimaye kumfutia leseni dereva, kuendelea kutoa elimu ya usalama

barabarani kwa njia mbalimbali,” ilieleza taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.

Kufuatiahali hiyo, wananchi wameomba njia za kutengeneza fursa za ajira za watu wengi ziongezwe ili kunusuru vijana. 

Reuben Masanja ambaye ni mwalimu mstaafu anasema kuendelea kutolewa kwa ajira itasaidia vijana wengi kuwa salama tofauti na hivi sasa wengi wameangukia kwenye bodaboda. 

“Unatafuta walimu wa shule za msingi sekondari, nenda kwenye bodaboda, inauma umesomesha mtoto anakuja kuwa bodaboda, fursa zitengenezwe nyingi watoto waajiriwe ili wawe salama” anasema Masanja.

Kwa mujibu wake, zamani bodaboda ilikuwa ni kazi inayofanywa na watu ambao walionekana kushindwa shule, lakini sasa imekuwa ni kazi ya wasomi.

Wakati hayo yakisemwa, tayari Serikali imetangaza ajira katika sekta mbalimbali ndani ya mwaka 2024 ikiwemo ualimu, afya na kwenye kada nyingine.