WAWAKILISHI wa Tanzania na visiwani Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, timu za Azam FC, Coastal Union, JKU na Uhamiaji, wameaga kirahisi mashindano hayo makubwa katika michezo ya awali tu.
Azam ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita nyuma ya mabingwa watetezi Yanga na mbele ya Simba, huku Coastal Union ikishiriki Kombe la Shirikisho kwa kumaliza katika nafasi ya nne.
Wawakilishi kutoka Zanzibar, mabingwa wa Ligi Kuu ya ZPL, JKU walicheza Ligi ya Mabingwa Afrika huku Uhamiaji FC ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kujikuta zote zikitupwa nje mapema.
Zipo sababu zilizochangia kutolewa mapema kwa timu zetu, kama ambavyo Mwanaspoti linazielezea.
Timu hii ilirejea kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mara ya kwanza 2015.
Mwaka 2015, timu hiyo ilishiriki baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-14, tena bila kupoteza mchezo wowote ambapo katika michezo 26, iliyocheza ilishinda 18 na kutoka sare minane chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog.
Azam FC iliyoanzishwa 2004 na kuanza kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008, licha ya kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika 2015, ilishindwa kutamba ikiishia hatua ya awali baada ya kuondoshwa na Al-Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex kushinda mabao 2-0, Februari 15, 2015, kisha ugenini kuchapwa 3-0, Februari 28, 2015.
Mwaka huo, bingwa alikuwa ni TP Mazembe ya DR Congo iliyoifunga USM Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya kuanza mchezo wa kwanza ugenini Algeria kwa ushindi wa 2-1, Oktoba 31, 2015, kisha kushinda Congo 2-0, Novemba 8, 2015.
Baada ya miaka 10, timu hiyo ikarejea tena ingawa imejikuta ikiendeleza rekodi yake mbovu ya kutovuka hatua inayofuata kufuatia kuondolewa mapema na APR FC ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1.
Azam ilianza kampeni zake kwenye Uwanja wa Azam Complex kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na nyota raia wa Colombia, Jhonier Blanco kwa penalti baada ya kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufanyiwa madhambi na beki wa APR, Claude Niyomugabo.
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa Rwanda, timu hiyo ikapoteza kwa kichapo cha mabao 2-0, na kuaga rasmi mashindano hayo huku dalili zikiwa zimejionyesha mapema tu kutokana na nafasi nyingi za kufunga zilizotengenezwa katika mechi ya kwanza.
Mchezo wa kwanza, Azam ilikosa utulivu katika kumalizia nafasi mbalimbali ilizotengeneza na kusababisha mechi ya marudiano kuwa ngumu kiasi cha kucheza na roho mkononi huku kocha wa kikosi hicho, Youssouph Dabo akiwa haepuki lawama kikosini.
Sababu nyingine iliyochangia ni kukosa maelewano mazuri katika safu ya kujilinda ya timu hiyo inayoundwa na mabeki wa kati, Yannick Bangala na Yeison Fuentes na eneo la ushambuliaji linaloongozwa na nyota mpya kikosini, Jhonier Blanco.
Katika michezo minne iliyopita ya mashindano ya timu hiyo kwa maana ya Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC imeruhusu mabao manane ikiwa na wastani wa kuruhusu mabao mawili katika kila mchezo mmoja huku ikifunga saba.
Eneo jingine ambalo Dabo aliifelisha Azam ni katika mabadiliko ya kikosi ambapo mara kwa mara amekuwa akibadilika japo sio mbaya kutokana na ubora, udhaifu wa mpinzani, lakini kwa kiasi kikubwa jambo hilo limemuangusha na kuruhusu mabao mengi.
Katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii ambayo timu hiyo ilichapwa mabao 4-1, dhidi ya Yanga Agosti 11, alionyesha mabadiliko ya kimfumo akiwaanzisha mabeki watatu wa kati nyuma na kusababisha eneo la ulinzi kufanya makosa mengi.
Sehemu nyingine iliyoifelisha timu hii ni katika eneo la beki ya kushoto ambako kwa kiasi kikubwa nyota wa kikosi hicho, Pascal Msindo aliyeonyesha kiwango kizuri msimu uliopita, alimpisha Cheikh Sidibe aliyeaminiwa katika mechi ya marudiano.
Sidibe alirejea wakati wa michezo ya mwishoni mwa msimu uliopita tangu alipopata majeraha Februari mwaka huu hivyo kiuhalisia bado hajapata mechi nyingi za kurudisha makali yake kama Msindo ambaye alionyesha kiwango bora hata mechi ya kwanza na APR.
Coastal imepata nafasi ya kushiriki michuano hii baada ya kumaliza katika nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita na licha ya kutotabiriwa makubwa ilionyesha dalili za kufeli mapema baada ya kuanza mgogoro na kocha wake, David Ouma.
Ouma alianza mgogoro na kikosi hicho katika suala la usajili wa nyota wapya msimu huu kiasi cha kusababisha kuvutana na viongozi ndani kwa ndani kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya waliosajiliwa tofauti na wale ambao yeye aliwapendekeza.
Mmoja wa pendekezo lake ni usajili wa kiungo Mkenya, Duke Abuya ambaye kwa sasa amejiunga na Yanga na beki wa kulia raia wa DR Congo, Djuma Shabani aliyetua Namungo ya Kocha Mwinyi Zahera, jambo ambalo halikumridhisha Ouma na kuanza mgogoro.
Mbali na hilo, Ouma aliwataka viongozi kuhakikisha wanabaki na beki wa kati Mkongomani, Felly Mulumba ambaye alipewa mkono wa kwaheri kisha kurejeshwa tena kikosini mwishoni na kutatua mapema suala la kipa, Ley Matampi kuhusu mkataba.
Matampi ambaye ni kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya kufikisha ‘clean sheets’ 15, alikuwa na matatizo ya kimkataba na kikosi hicho ambacho kilidai alikuwa na mkataba zaidi wa mwaka mmoja huku yeye mwenyewe akieleza sio kweli.
Matatizo hayo yalifanya kipa huyo kutokuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mechi za Ngao ya Jamii ilizopigwa 5-2 na Azam na 1-0 na Simba na kisha kupasuka 3-0 ugenini Angola dhidi ya Bravos do Maquis katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya kichapo hicho, viongozi wa timu hiyo wakamtimua Ouma kwa kile walichokieleza kusikitishwa na matokeo ya kikosi hicho huku wakimalizana na Matampi na kumrejesha katika mchezo wa marudiano ambao uliisha kwa suluhu hivyo kutupwa nje.
Mambo hayo yameifanya Coastal kurudia historia iliyoiweka mwaka 1989, iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza kabla ya michuano hiyo kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.
Mwaka huo, Coastal ilitolewa kwa jumla ya mabao 4-0, dhidi ya Mbabane Highlanders FC ya Eswatini baada ya kulala 2-0, nyumbani na ugenini hivyo kutupwa nje mapema.
Kipindi hicho bingwa ilikuwa ni Raja Casablanca ya Morocco iliyoifunga Mouloudia Club Oran (MC Oran) ya Algeria kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya kila timu kushinda kwake kwa bao 1-0.
Timu hizi zilionyesha mapema tu dalili za kutolewa katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho baada ya kuchagua michezo yake yote kuichezea ugenini kwa maana ya JKU iliyochagua kuchezea Misri na Uhamiaji ikichagua Libya.
Kuonyesha hilo, JKU ilianza kampeni zake katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kichapo cha mabao 6-0, dhidi ya matajiri wa Misri, Pyramids FC kisha marudiano kuchapwa 3-1, hivyo kuaga michuano hiyo mapema tu kwa kutolewa kwa jumla ya mabao 9-1.
Uhamiaji iliyokuwa inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ilichezea michezo yake yote miwili Libya ambako mechi ya kwanza ilichapwa mabao 2-0, dhidi ya Al-Ahli Tripoli huku marudiano ikichapwa 3-1 na kutolewa kwa jumla ya 5-1.
Sababu kubwa iliyochangia timu hizo kucheza michezo yote ugenini ni kitendo cha kocha mkuu wa JKU, Haji Salum kunukuliwa akisema, wamepata udhamini wa kulipiwa gharama za safari ya Misri, gharama za kambi na gharama za kufanya utalii Misri.
Mbali na hilo ila walilipiwa gharama za uwanja wa mazoezi, gharama za mafunzo kwa makocha na pia kuiingiza shule ya soka ya jeshi hilo kwenye program za klabu ya Pyramids, jambo ambalo ilikuwa ni wazi walijipanga kushindwa na sio kushindana.
Kwa miaka mingi, timu nyingi za Afrika zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho zinaamini nyumbani ndio sehemu pekee ya ushindi ingawa haina maana hauwezi kupoteza japo kwa wawakilishi wetu hawakuwa na malengo zaidi ya hapo.
Kocha wa Azam FC, Dabo ambaye kwa sasa amekalia kuti kavu ndani ya timu hiyo anasema, wachezaji walicheza kwa presha tangu mchezo wa kwanza na kusababisha kukosa utulivu.
“Inauma ila ndio mpira wa miguu ulivyo, kuna muda unapata kile ambacho haukukitarajia, tunaendelea kujifunza kutokana na makosa na naamini tutakuwa bora zaidi huko mbele, japo haikuwa malengo yetu kutolewa hatua hii ya awali,” anasema.
Kaimu kocha mkuu wa Coastal, Ngawina Ngawina anasema, malengo yao yalikuwa kuvuka hatua inayofuata lakini kushindwa kuwasoma vyema wapinzani wao katika mchezo wa kwanza kuliwagharimu.