AKILI ZA KIJIWENI: Simba Queens imevuna ilichokipanda

MATUMAINI yalikuwa makubwa sana kwa Simba Queens kwamba ingetwaa ubingwa wa mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa wanawake yaliyofikia tamati jana huko Ethiopia.

Mashindano hayo yako chini ya usimamizi wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na bingwa wake hupata moja kwa moja tiketi ya kushiriki klabu bingwa Afrika kwa wanawake.

Wengi tuliamini Simba Queens ingefanya vizuri katika mashindano hayo kwa sababu tatu za msingi ya kwanza ikiwa ni uzoefu ambao imekuwa nayo kulinganisha na timu nyinginezo za wanawake katika ukanda huu.

Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa Simba Queens kushiriki mashindano ya Cecafa ya kuwania kufuzu klabu bingwa Afrika kama ilivyo kwa CBE ya Ethiopia, pia Kawempe Muslim ya Uganda yenyewe imeshiriki mara ya pili.

Sababu ya pili ni ubora wa kikosi ilichonacho kinachoundwa na wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa kutoka mataifa mbalimbali tena yanayofanya vyema katika soka la wanawake kama vile Nigeria, Kenya na Ghana.

Na jambo la tatu ni mwanzo mzuri ambao Simba Queens ilianza nao katika mashindano hayo ya kufuzu mwaka huu ambapo katika mechi ya kwanza ilifunga mabao manane na kutoruhusu lolote katika mechi mbili za mwanzo ilizocheza na FAD ya Djibouti na Kawempe Muslim ya Uganda.

Hata hivyo, ikapoteza mechi ya nusu fainali dhidi ya Police Bullets ya Kenya kwa kufungwa mabao 3-2 katika mchezo ambao ulitawaliwa zaidi na makosa binafsi ya wachezaji na jambo linaloashiria kuwa waliridhika na mafanikio ambayo waliyapata hapo nyuma.

Wachezaji wa Simba Queens hasa wanaocheza katika nafasi za ulinzi wanapaswa kuwajibika na kufanya kwao vibaya katika mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati kwa wanawake.

Washambuliaji wanaweza kujitetea kidogo kwa vile wao wamefunga mabao katika kila mechi katika mashindano hayo tofauti na wale wa nafasi za ulinzi ambao wamefanya waonekane kazibure.

Related Posts