BAADHI ya wachezaji wa timu za Ligi Kuu Bara wamedai kushtushwa na kusikitishwa na hali aliyonayo sasa nyota wa zamani wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu, kuendelea kuteseka na kushindwa kufanya majukumu ya kifamilia na kisoka kwa ujumla.
Mwanaspoti lilibua hali ya Mdamu baada ya kumtembea nyumbani kwake Kimara Bonyokwa, ambako alifunguka kwamba bado anahitaji msaada wa Watanzania kumchangia pesa ya matibabu kutokana na jeraha la kuvunjika mguu wakati akitoka kwenye mazoezi ya Polisi Tanzania miaka mitatu iliyopita kumtesa.
Julai 9, 2021 basi la timu ya Polisi Tanzania, lilipata ajali likitoka katika mazoezi Uwanja wa TPC kwenda kambini, ambako Mdamu alivunjika miguu yote miwili, jambo ambalo liliwagusa Watanzania wengi kujitoa kwa ajili ya matibabu yake, hata hivyo hakupona kabisa.
Kiungo wa Singida Black Stars, Zawadi Mauya baada ya kuona taarifa za Mdamu katika gazeti la Mwanaspoti alisema; “Tunashukuru kwa kuliibua jambo hilo, tulidhani amepona, kumbe bado anaishi kwa mateso hadi muda huu, tunawaomba msichoke kuwajulisha Watanzania ili apate msaada wa kutibiwa.”
Kiungo huyo mkabaji wa zamani wa Kagera Sugar na Yanga, aliongeza; “Sisi wachezaji tunaweza tukawa tunamtumia pesa ya chakula baada ya kujua hali yake, lakini hilo halitoshi kinachotakiwa ni afya yake kuimalika ili aweze kulea watoto wake.”
Hoja hiyo ya Mauya, iliungwa mkono na mshambuliaji wa Azam FC, Adam Adam aliyesema; “Imenishtua kuona mshikaji bado anaendelea kuteseka, Mwanaspoti ni gazeti kubwa, msichoke kuendelea kuwajuza watu hali yake, naamini wapo ambao wanaweza wakajitoa kwa ajili ya kuokoa maisha yake, kama wachezaji tunaweza tukawa tunajitoa ili asikose ya kula, ila bado tutakuwa hatujatibu tatizo.”
Kwa upande wa mshambuliaji wa JKT Tanzania, Charles Ilanfya alisema “Binafsi huwa najitoa kumpa chochote kitu, lakini ni lazima atibiwe.”