KIKOSI cha Singida Fountain Gate kilichopo Ligi Kuu Bara, leo Jumamosi kinashuka kwenye Uwanja wa nyumbani wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara ili kutesti mitambo dhidi ya maafande wa Mbuni waliopo Ligi ya Championship.
Mechi hiyo inatumiwa na timu zote kujiandaa na mechi zao za ligi inazoshiriki, Fountain ikijiandaa kuipokea KenGold ya Mbeya mchezo utakaopigwa Septemba 11, wakati Mbuni inajiandaa na Championship itakayoanza mwishoni mwa mwezi huu.
Fountain iliyocheza mechi mbili za Ligi Kuu ya msimu huu ikipoteza moja kwa mabao 4-0 mbele ya Simba na kushinda 2-0 dhidi ya Namungo, ipo chini ya kocha Mohammed Muya aliyeliambia Mwanaspoti kuwa, bado anaendelea kujenga kikosi chake na kwa asilimia kubwa amebaini mabadiliko mengi anapambana kurekebisha dosari zilizopo kwa lengo la kuifanya iwe na ushindani zaidi na sio kugawa pointi.
Alisema mchezo dhidi ya Mbuni anautumia kurudisha utimamu wa wachezaji waliopata mapumziko kutokana na uwepo wa mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazowania tiketi ya Afcon 2025.
“Baada ya ushindi dhidi ya Namungo nilitoa mapumziko kwa wachezaji tumerudi kambini wiki hii tumeanza mazoezi ya gym sasa tumerudi uwanjanji na nimeomba mchezo mmoja kabla ya kuikaribisha Ken Gold Jumatano,” alisema Muya na kuongeza;
“Nitautumia mchezo huo kuwaweka kwenye mazingira mazuri na ya ushindani wachezaji wangu ili kuutumia vyema uwanja wa nyumbani na kukusanya pointi za kutubakisha msimu ujao kwenye michezo ya mzunguko wa kwanza.”
Muya alisema mchezo na KenGold iliyopanda daraja msimu huu na iliyoanza kwa kufungwa 3-1 na Singida Black Stars, utachezwa katika Uwanja wa Tanzanite.