Kauli za Msigwa zilizomuibua Mbowe kudai fidia ya Sh5 bilioni

Tanga. Uamuzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe kutangaza nia ya kumburuza mahakamani Mchungaji Peter Msigwa kutokana na kauli dhidi yake, umemwibua mchungaji huyo akisisitiza baadhi ya kauli hizo, na kuwa yuko tayari kukutana naye mahakamani.

Mchungaji Msigwa alijivua uanachama wa Chadema Juni 30, 2024 na kuhamia CCM na tangu wakati huo amekuwa akitoa kauli dhidi ya Chadema na Mbowe katika majukwaa ya kisiasa na kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Kwa muda mrefu, Mbowe amekuwa kimya huku Msigwa akisisitiza ajitokeze kujibu badala ya masuala hayo badala ya kuyapeleka mahakamani, ambako pia amesema, kuwa yuko tayari kwa hatua hiyo.

Mbowe ametangaza nia hiyo katika taarifa ya madai aliyomwandikia Msigwa kupitia jopo la mawakili watano, iwapo hatatekeleza masharti aliyompa ndani ya siku tano yanayohusisha kuomba radhi kwa kauli hizo anazosema zina lengo la kumshushia hadhi.

Katika notisi ya Mbowe kwa Mchungaji Msigwa zimeorodheshwa kauli mbalimbali ambazo anadai mchungani huyo amekuwa anazitoa kwa nia ovu dhidi yake.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile ya Juni 30, 2024 aliponukuriwa na Mwananchi Digital na Channel Ten akisema:

“Mtu mmoja amegeuza chama kinakuwa Saccos, mtu mmoja, mwenyekiti wa maisha hataki kugombania na mtu yeyote, anagombea ueneyekiti wa chama pekee yake, anataka kugombea urais mwenyewe, wenyeviti wa kanda anaowataka yeye, hicho hakiwezi kuwa chama cha familia, hiki ni chama cha taasisi, kinatakiwa kifuate misingi.

“… niseme kwa kifupi kwamba mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo hafai kuaminiwa, he’s not supposed to be trusted, ukimuangalia tu hata anapohutubia hana ujasiri, amekosa nuru, hafai kuaminiwa…”

Kauli nyingine ni zile anazodaiwa kuzitoa Julai 19, 2024 katika mkutano uliofanyika Mwembetogwa, Iringa kuwa:

“Mheshimiwa Mbowe anatumia sekretarieti ya chama kwenye private office. Ana kitu kinaitwa Mbowe Foundation na hii ni kinyume na utaratibu, huwa mnasikia Nyerere Foundation, Mkapa Foundation, Kikwete Foundation, mshawahi sikia Samia Foundation?”

“Foundation huwa zinaanzishwa ukishatoka madarakani, kwa sababu hamtakiwi kuwa na masilahi nazo, yeye ameanzisha kitu kinaitwa Mbowe Foundation, michango yote badala iende kwenye chama inakuwa channelled kwenda Mbowe Foundation, kwenye akaunti ya chama pesa haziendi.”

“…Mnapokuwa kwenye chama kwa sababu wanachama hawachangii kwenye Mbowe Foundation, inapelekwa kwake, utasikia ‘mimi’ sasa nitakikopesha chama’. Tukianza operations akaunti za chama hazina hela, Mbowe Foundation imechukua zote”

“Ndo mnamuona yeye anaruka na helicopter, anatembea na fleet ya magari kumi (10), anabeba mpaka podium kwenye gari, mwenzake Tundu Lissu na ulemavu wake anatembea kwenye kagari kamoja ka kukodi”

“… Na hili la pili, kwa hiyo Mbowe Foundation imekusanya hela haziendi, na sekretarieti nzima ya chama inafanya kwenye private office ya Mbowe kinyume na ethics, lakini siyo utaratibu.

Pia Mchungaji Msigwa akimtaja Mbowe kama Bwana mkubwa pia alitamka kuwa:

“Kwenye huu ufisadi, Chadema mnaziona hizi, kuna kitu kinaitwa Chadema digital sio mali ya chama, inamilikiwa na kampuni moja iko Kenya, na Bwanamkubwa yeye ni shareholder kwenye hiyo kampuni. Muulizeni Mnyika (John, Katibu Mkuu wa Chadema) kama Chadema digital ni ya chama.”

Vilevile Mchungaji Msigwa anadaiwa Julai 24, 2024 katika jukwaa la mtandaoni liitwalo Chumba cha Taifa Kwanza Hajji305 (Club House Room) wakati akijibu maswali ya wasikilizaji alisema kuwa:

“…kwamba eeh! Mheshimiwa Mbowe ana Mbowe Foundation hiyo siyo siri anayo, namna hiyo hiyo Mbowe Foundation ndio actually ina run chama sasa hivi.

“Kama nilivyosema, nasisitiza kabisa eeh! Inarun chama na ndio maana enh, haiwezekani kama ni chama kimoja chenye kusimamia mambo yanayofanana, eeh! Mwenyekiti awe na helikopta atembee na fleet ya magari zaidi ya 10.

“Kwa hiyo hata mipango ya operation inaratibu Mbowe Foundation na sekretarieti kuna baadhi ya watumishi wanafanya kwenye Mbowe Foundation na sekretarieti.

“… eeh na sekretarieti watu kama kina Reg na Mrema ndio wanakuwa kwenye Mbowe Foundation zaidi kwa sababu ndio kunakuwa kuna hela zaidi huku kwenye Chadema kunakuwa na ukata. Mbowe anapata michango ya chama inawekwa kwenye Mbowe Foundation.”

“Mwenyekiti Mbowe juu ya wabunge 19 ana mahusiano nao, wanalipa kitu kidogo na kwamba sasa hivi anajitajidi kuwarudisha kwenye mlango wa nyuma na jambo hilo linaleta shida sana kwenye Bawacha (Baraza la Wanawake Chadema). Mheshimiwa Mbowe ndiye alihusika kuwapeleka bungeni.”

“Kimsingi mimi nawasaidia Chadema mjenge chama chenu, kwa uongozi wa Mbowe chama hakipo wala sio taasisi tena, ile nimezungumza kwamba sekretarieti imepararaizi, inafanya kazi ya Mbowe Foundation haifanyi kazi ya chama, haipati matatizo kutoka kwa Mnyika hapo huelewi wapi mnataka nisemeje.”

“Mbowe ametengeneza mazingira ya kutosha wengine na yeye anajua Chadema ni project ya Mbowe.”

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa Julai 27, 2024 Mchungaji Msigwa alifanya mahojiano na Mwanahalisi TV na inamnukuu maneno anayodaiwa kuyasema kuwa:

“Mwenyekiti wa Chama cha Chadema yeye alivyoitwa alituacha mahakamani wafuasi wake akakimbia kwenda ikulu hata koti hajanyoosha.”

“Katika ule uchaguzi wa Kanda ya Nyasa nilikuwa sishindani na Sugu, bali nilikuwa nashindana na Mbowe.”

“Anakuwa na mwenyekiti wa chama ambaye haongei na wenyeviti wa kanda zaidi ya miezi mitano, haongei na wenyeviti wa mikoa zaidi ya miezi mitano, hawasiliani na yeyote, makatibu wa kanda wana hali ngumu, huyu ni mwenyekiti wa nini.”

“Lissu, Heche Lema mwenyekiti Mbowe ana mpango wa kuwaondoa kwa sababu wana uelewa, wanahoji, wana critical thinking.”

Vilevile yamo maneno anayodaiwa kuyatamka Agosti 17, 2024 katika mkutano wa hadhara Katoro kuwa:

“Mbowe amezungukwa na wahuni.”…

“Lakini siku hiyo natoka gerezani amekaa hivi analia kabisa anatoa machozi anasema Msigwa usiende, usiende, kama mtu mwema, kaka kanitolea pesa anasema Msigwa usiende. Sio alikuwa analia kwa sababu anataka nisiende, alikuwa analia kwa sababu anaona nikienda CCM atakosa mtu wa kumtumia.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maneno yake hayo (Msigwa) ya uongo, na ya nia ovu na ya kashfa dhidi ya Mbowe, yanalenga kuharibu hadhi, uadilifu, utu na heshima binafsi ya mteja wao na kumjengea picha kama mtu mpotofu.

Wanasisitiza kuwa yanamharibia mteja wao  taswira na sifa njema jumuiya ya wafanyabiashara, jumuiya ya kidini, na ulimwenguni kote aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 50 kama mkristo, baba wa familia, mfanyabiashara na kiongozi wa kisiasa.

Vilevile wanadai kuwa kitendo cha Mchungaji Msigwa kurudiarudia kauli hizo zinazokusudia kumkashfu mteja wao kimeendelea kuathiri hadhi ya mteja wao  katika macho ya umma, jumuiya ya wafanyabiashara na duniani kote kwa kuwa yamechapishwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambako zinadumu.

Hivyo mawakili hao wanadai kuwa kauli hizo za kashfa si tu zimedhuru hadhi ya mteja wao binafsi, bali hata familia yake, marafiki wa kisiasa, kibiashara, kidini.