WAKATI Ken Gold ikitarajia kushuka uwanjani Jumatano uwanjani kuwakabili Fountain Gate, benchi la ufundi limesema halitarajii kuruhusu tena bao badala yake ni kutembeza vipigo baada ya kukisuka upya kikosi.
Ken Gold inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza haikuwa na mwanzo mzuri baada ya kukandwa kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars na keshokuta watakuwa kibaruani dhidi ya Fountain Gate huko Manyara.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza, ambapo wenyeji Fountain Gate wamecheza mechi mbili wakipoteza mmoja dhidi ya Simba kwa 4-0 kisha kushinda mbele ya Namungo mabao 2-0.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema baada ya kuanza vibaya walitathimini walipokosea na muda waliokaa mapumziko wamerekebisha makosa na sasa wanaenda kuianza upya ligi.
Alisema wanafahamu mechi haitakuwa rahisi, lakini kwa namna alivyoisuka timu yake kuanzia eneo la nyuma, kati na mbele, Ken Gold inaenda kufanya vizuri na kwamba hawatarajii kufungwa tena mabao.
“Mechi ya kwanza ilitupa somo tukajitathimini na kusahihisha tulipokosea, tumekuwa na muda mzuri wa maandalizi na timu imeimarika na sasa tunaenda kuianza upya ligi”
“Vijana wana ari na morali, tutawaheshimu wapinzani na matarajio yetu ni kushinda ili kurejesha morali ndani na nje ya uwanja, tunaenda kuanza na Fountain Gate kupata muelekeo rasmi” alisema Kocha huyo.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Jose Mkoko alisema hadi sasa hakuna mchezaji mwenye tatizo lolote kuweza kukosa mchezo huo na kilichobaki ni uamuzi wa benchi la ufundi kuamua nani aanze au kusubiri.
“Vibali kwa wachezaji wote vimetimia, hakuna mwenye tatizo lolote aidha kadi au majeruhi, timu inatarajia kuandoka Jumapili (jana) tayari kwa mchezo na wapinzani wetu” alisema Mkoko.