WAKATI Ligi ya Championship ikitazamiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni kwa mwezi huu Chama Cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA) imeweka wazi kuwa imejipanga kutoa sapoti ya kutosha kwa timu zake Mbuni FC na TMA Stars ili kufanya vyema na kupanda daraja.
Mara ya mwisho kwa Arusha kuwa na timu ya Ligi Kuu ilikuwa ni mwaka 2014 miaka 10 iliyopita kupitia timu ya Jkt Oljoro ambayo nayo msimu huo wa 2013/14 ilishuka daraja.
Baada ya hapo Mkoa huo ikajipapatua kupitia timu zake zilizokuwa Championship wakati huo ambazo ni Jkt Oljoro,Arusha United na AFC Arusha kutaka kurejea Ligi Kuu lakini zikaishia kupotea kwenye ramani ya Soka.
Na sasa Arachuga ina timu mbili za Mbuni FC ambayo inashiriki Championship kwa msimu wa tatu na TMA Stars ambayo ni msimu wake wa pili,timu zote zinamilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Akiongea na Mwanaspoti,Mwenyekiti wa ARFA,Zakayo Mjema alisema kama chama wameandaa mikakati mizuri ya kuhakikisha wanazipa sapoti timu hizo ambazo anaamini itazifanya kupanda daraja na kurejesha heshima ya Arusha.
Alisema wanariadhishwa na usajili ambao umefanywa na timu hizo mbili kwa maana ya kusajili wachezaji wengi ambao wana uzoefu na Ligi ngumu ya Championship hivyo sasa kazi iliyobaki na kuongeza ushirikiano ili kuzipandisha.
“Timu zetu ni nzuri kikubwa wadau wazipe sapoti ya kutosha ili ziweze kupanda ambapo itakuwa heshima kwetu lakini pia itakata kiu ya mashabiki ambao wanatamani kuona timu hizi zikipanda”,alisema Mjema.
Alisema tayari wamekutana na viongozi wa timu hizo kujadili namna gani ya kushirikiana ili kuweza kufanya vizuri na kuzipandisha daraja.