Dar es Salaam. Wakati watahiniwa 1,230,780 wakitarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) kesho, Baraza la Taifa la Mtihani (Necta) limewatahadharisha watahiniwa wanaopanga kufanya udanganyifu, watafutiwa matokeo.
Mtihani huo unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili nchi nzima, utaanza kesho Septemba 11 na kumalizika Septemba 12, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo leo Jumanne Septemba 10, 2024, Katibu mtendaji wa baraza hilo, Said Mohamed amesema katika watahiniwa 1,230,780 wasichana ni 564,176 sawa na asilimia 45.84 na wavulana ni 666,604 sawa na asilimia 54.16.
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosailiwa kufanya mtihani huo ni 4,583 kati yao 98 ni wasioona, 1402 wenye uoni hafifu, 1,067 wenye uziwi, 486 ni wenye ulemavu wa akili na 1530 ni wenye ulemavu wa viungo.
“Kati ya watahiniwa 1,230,780 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2024, watahiniwa 1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani wa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya mtihani wa lugha ya kiingereza,” amesema katibu huyo.
Kuhusu masomo watakayotahiniwa, amesema ni sita ambayo ni Kiswahili, kiingereza, sayansi na teknolojia, hisabati, maarifa ya jamii, stadi za maisha pamoja na uraia.
Mohamed amewaonya watahiniwa wanaopanga kufanya udanganyifu, akisema watafutiwa matokeo.
“Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri watahiniwa wote katika kipindi chote cha miaka saba ya elimu ya msingi.
“Aidha baraza halitarajii kuona mwanafunzi yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na mwanafunzi atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mtihani,” amesema.
Kwa upande wa wasimamizi wa mitihani amewataka kufanya kazi hiyo kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu ikiwamo kuhakikisha wenye mahitaji maalumu wanapata haki yao ya msingi.
“Haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu.
“Aidha, watahiniwa wenye mahitaji maalumu waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati na dakika kumi kwa kila saa kwa masomo mengine kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza,” amesema.
Akielezea kuhusu maandalizi, Mohamed amesema yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo kutoka halmashauri na manispaa zote nchini.
“Kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu kwa kutoa semina kwa wasimamizi wa mitihani pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,” amesema.
Amezitaka kamati za mitihani zihakikishe kuwa usalama wa vituo vyote vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza.
Kwa upande wa wamiliki wa shule amewataka kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo.
Ametaka kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu ikiwamo kuheshimu eneo la mtihani kwa kuepuka mtu kuingia maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani.