Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) na nyenzo za usimamizi wa uwekezaji nchini, jijini Dar es Salaam kesho Jumatano Septemba 11, 2024.
Pia, atazindua taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2023 na mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa kanda maalumu za kiuchumi nchini pamoja na mpango mkakati wa ofisi ya Rais, mipango na uwekezaji.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 10, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alipozungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
Profesa Kitila amesema Juni 2019, Serikali ilizindua rasmi Mkumbi huku ikilenga kufanya uchambuzi wa mazingira ya biashara nchini.
Amesema lengo lingine lilikuwa ni kuainisha mageuzi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kutatua changamoto na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.
“Tunatarajia kesho Waziri Mkuu Majaliwa, atamwakilisha Rais Samia katika uzinduzi wa mpango huo ambao pamoja na masuala mengine, atazindua taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2023 katika sekta mbalimbali,” amesema.
Profesa Kitila amesema Mkumbi uliainisha maeneo makubwa matatu ya kushughulikia katika kuboresha mazingira ya biashara nchini.
“Maeneo hayo ni gharama za kufanya biashara, mlolongo mgumu na mrefu wa kupata vibali vya kufanya biashara na uwepo wa utitiri wa mamlaka za udhibiti zinazorekebu shughuli za biashara nchini,”amefafanua.
Kutokana na changamoto hizo, amesema Serikali iliajiri mtaalamu mshauri kufanya tathmini huru na ya kina ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mkumbi na kufuatia kukamilika kwa taarifa hiyo itazinduliwa kesho.