BAADA ya kushindwa kutamba katika marathoni za Olimpiki zilizofanyika Paris, Ufaransa mwaka huu, mwanariadha Gabriel Geay amesema kuwa nguvu zote kwa sasa amezielekeza kwenye mbio za New York City Marathon.
Akizungumza na Mwanaspoti, Geay alisema japokuwa ni mara ya kwanza kushiriki mbio hizo, lakini anaamini atakwenda kufanya vizuri kulingana na namna ambavyo anaendelea kufanya mazoezi.
Aliongeza kuwa hana wasiwasi na wanariadha ambao anashindana nao kwani ni walewale ambao amekuwa akikutana nao katika mbio zingine ambapo amekuwa akishindana nao na wakati mwingine kuwashinda.
“Naamini nitaenda kufanya kitu kikubwa ambayo haijawahi kushuudiwa New York kama nitakuwa fiti kwa asilimia zote lazima nitashinda”, alisema Geay.
Geay anakwenda kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye mbio hizo za nchini Marekani ambazo zinafanyika kwa mara ya 54 tangu zilipoanzishwa 1970 zikitarajiwa kutimua vumbi Novemba 3.
Bingwa huyo mwenye rekodi ya marathoni ya taifa kwa muda wa saa 2:03:00, rekodi ambayo aliiweka 2022 kupitia mbio za Valencia Marathon, katika mbio za New York City atakutana na ushindani mkubwa kutoka kwa nyota mbalimbali wakiwamo mshindi wa mbio hizo 2023, Tamirat Tola ambaye pia ni mshindi wa marathoni za Olimpiki za Paris 2024 pamoja na mshindi mara mbili wa Boston Marathon, Evans Chebet.
Nyota wengine ni Geoffrey Kamworo, Abel Kipchumba, Albert Korir, Wesley Kiptoo wote kutoka Kenya, Bashir Abdi (Ubelgiji), Abdi Nageeye (Uholanzi), Elkanah Kibet, Clayton Albertson (Marekani), Callum Hawkins (Uingereza) na Addisu Gobena waa Ethiopia.