KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata, raia wa Uganda amesema baada ya kucheza michezo miwili ya ligi na kupoteza yote, sasa wamejipanga kupambana kufa au kupona ili kuanza kukusanya pointi huku akiamini kwamba rekodi ya msimu uliopita itawabeba dhidi ya Tabora United.
Kauli ya kocha huyo imekuja ikiwa kesho Jumatano anatarajia kukiongoza kikosi chake kucheza dhidi ya Tabora United katika mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mchezo huo utakaoanza saa 8:00 mchana utachezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo msimu uliopita timu hizo zilipokutana hapo, Kagera Sugar ilishinda 3-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nkata amesema timu hiyo imefanyia kazi mapungufu yaliyokuwepo ambapo kwa maandalizi yaliyofanyika anaamini watapata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo.
“Tumecheza mechi mbili kabla na tumepoteza zote, bahati mbaya tumepoteza tukiwa nyumbani lakini kuelekea mchezo dhidi ya Tabora United tumejiandaa vizuri na tunaamini tutapata matokeo mazuri kwenye mechi hii utakayochezwa saa nane mchana hapa Tabora.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu kwa kuwa wametoka kupata ushindi tena ugenini, tunatambua kwamba watakuja na nguvu zaidi lakini kwa msimu uliopita tulipata matokeo mazuri dhidi yao kwa hivyo tunaamini hata sasa inawezekana,” alisema.
Wakati Nkata akiyasema hayo, Kocha Mkuu wa Tabora United, Francis Kimanzi amesisitiza kwamba maandalizi kwa upande wao yamekamilika na wapo tayari kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar.
“Tumejiandaa na tuko tayari kwa mchezo, kushinda ugenini dhidi ya Namungo ilitupa kujiamini ili tuje nyumbani kupambana na tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa hamasa timu yao kwakuwa kila mchezo kwetu ni fainali,” alisema kocha huyo.
Mpaka sasa Kagera Sugar imecheza mechi mbili kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Black Stars na kufungwa bao 1-0, kisha ikapokea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga zote ikicheza nyumbani Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Kwa upande wa Tabora United, ilianza ligi kwa kufungwa mabao 3-0 na Simba kisha ikashinda mabao 2-1 mbele ya Namungo ugenini.
Msimu uliopita ambao timu hizo zilikutana mara ya kwanza kwenye ligi, Kagera Sugar waliibuka wababe wakishinda 3-0 Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi baada ya mzunguko wa kwanza nyumbani kwao Kaitaba matokeo kuwa 0-0.
Timu hizo ambazo zote zimeshuka dimbani mara mbili msimu huu, katika msimamo wa ligi Tabora United ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi tatu, wakati Kagera Sugar ikiburuza mkia bila ya pointi.
Katika mchezo mwingine wa ligi leo Jumatano kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, Fountain Gate FC itaikaribisha KenGold.
Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kuchezwa mkoani humo ikiwa ni historia kwa wananchi wa eneo hilo kuanza kushuhudia mechi za Ligi Kuu.
Fountain Gate kutokea Dodoma, imeamua kuutumia uwanja huo kwa mechi za nyumbani msimu huu.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema baada ya kucheza ugenini mechi mbili, sasa wanarudi nyumbani kuonyesha ubabe wao.
“Hii ni mechi yetu ya kwanza nyumbani msimu huu, lazima tufanye kitu kwa mashabiki wetu na wakazi wa mkoani hapa kwa ujumla, hivyo tumejiandaa vizuri kushinda,” alisema kocha huyo ambaye katika mechi mbili za ugenini, alianza kwa kufungwa 4-0 na Simba, kisha akashinda 2-0 dhidi ya Namungo.
KenGold ni wageni katika ligi wakishiriki kwa mara ya kwanza msimu huu, hawaanza vizuri kwani mechi moja waliyocheza nyumbani wamepoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, huu ni mchezo wa pili kwao.