JAHAZI la Kagera Sugar linazidi kuwenda mrama baada ya mchana wa leo kufumuliwa bao 1-0 na Tabora United, ikiwa ni kipigo cha tatu mfululizo kwa timu hiyo inayonolewa na kocha kutoka Uganda, Paul Nkata.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Nyuki wa Tabora, baada ya awali kuitungua Namungo ikiwa ugenini mjini Lindi kwa mabao 2-1 na kuifanya sasa ifikishe pointi sita kutokana na mechi tatu za msimu huu ikizishusha timu kadhaa katika msimamo ikiwamo Yanga na kukwea hadi nafasi ya tatu.
Katika mechi hiyo iliyopigwa saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini hapa, wenyeji walionyesha dhamira ya kusaka pointi tatu za kwanza nyumbani kutokana na kuanza kwa kasi na kupata bao hilo pekee dakika ya 32 tu ya mchezo huo lililowekwa kimiani kwa mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji wa Tabora, Yacouba Songne kufanyiwa madhambi na ndani ya eneo hatari na beki wa Kagera, Saleh Seif na mwamuzi Ramadhan Kayoko ipigwe na Asiedu Shedrak akaukwamisha wavuni mbele ya kipa Ramadhan Chalamanda aliyekuwa langoni mwa wageni. Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko, licha ya kila timu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka mabvao bila ya mafanikio.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, Kagera ikisaka bao la kusawazisha, huku wenyeji wakitafuta jingine, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wa timu hizo ulifanya hadi dakika 90 zilipomalizika matokeo kuwa ushindi huo wa 1-0 kwa Tabora, huku Kagera ikiangusha penalti nyingine baada ya awali kupoteza nyumbani dhidi ya Singida BS na Yanga.
Kivutio katika mchezo huo alikua kiungo wa Tabora United Asiedu Shedrak ambaye alimudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji ambaye alizima ubora cha kiungo wa Kagera, Nassoro Kapama aliyekuwa na kiwango cha juu kwa mechi za karibuni.
Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Tabora, Mkenya Francis Kimanzi aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kufanya kile alichowaagiza kwa ubora na kupata alama tatu muhimu.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi dhidi ya Kagera Sugar, kama mlivyoona mchezo ulikua na ushindani mkubwa na wachezaji wamefanya kile tulichowaagiza na tumepata matokeo naamini imetupa kujiamini zaidi kuelekea michezo inayofuata,” amesema Kimanzi na kuongeza;
“Kwa msimu uliomalizika Kagera Sugar walipata alama nne kwetu lakini msimu huu tumeanza kwa kupata ushindi kwenye uwanja wetu wa nyumbani hii ni ishara kwamba tumefuta uteja dhidi yao na yale makosa ambayo tumeendelea kuyafanya tutayafanyia kazi ili tuwe na timu imara zaidi.”
Kwa upande wa kocha wa Kagera, Paul Nkata aliyeshuhudia timu hiyo ikipoteza pointi tisa katika mechi tatu za awali, amesema timu hiyo haikuwa na bahati licha ya wachezaji kujituma.
“Kwenye mchezo huu hatukuwa na bahati kwani tangu mwanzo wa mchezo tumetengeneza nafasi kadhaa ambazo tumeshindwa kuzitumia hivyo tunarejea nyumbani, makosa ambayo yamekuwa yakitokea kwa kujirudia tutayapunguza ili tuweze kupata matokeo,” amesema Nkata na kuongeza;
“Kupoteza mechi tatu mfululizo sio ishara nzuri kwetu na huwa haizoeleki na hayakuwa malengo tangu kuanza kwa ligi kwa mantiki hiyo tutaendelea kufanyia kazi mapungufu yetu ili tuweze kupata matokeo kwenye mechi zijazo.”