DC Shaka aunda kamati kuchunguza kifo cha mjamzito

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro (DC), Shaka Hamdu Shaka ameunda kamati kuchunguza chanzo cha kifo cha mjamzito kinachodaiwa kusababishwa na kucheleweshewa huduma.

Amechukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Seleman Makuani, ambaye amedai mke wake Zaituni Mayuga alipoteza maisha baada ya kucheleweshewa huduma akitakiwa kutoa Sh180, 000 kujaza mafuta gari la wagonjwa litakalomsafirisha mkewe kwenda Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Mikumi.

Shaka aliyekuwa kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika Kata na Kijiji cha Kidodi, Jumatatu, Septemba 9, 2024 amesema lengo la kamati hiyo ni kubaini ukweli ili haki iweze kutendeka, itakapobidi sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha matukio ambayo yanaondoa huruma, utu na ubinadamu.

Katika mkutano huo, Makuani alidai mke wake alicheleweshewa huduma ya kusafirishwa kutoka Kituo cha Afya Kidodi kwenda Hospitali ya Mtakatifu Kizito kutokana na kukosa Sh180,000 za mafuta ya gari.

Kwa mujibu wa maelezo ya Makuani, walipatiwa huduma hiyo baada ya kutoa Sh100, 000,  ndipo aliposafirishwa huku muda mrefu ukiwa umepita.

Kutokana na malalamiko hayo, Shaka amesitisha mkutano wa hadhara na kuitisha kikao cha kamati ya usalama ya wilaya kwa dharura kutafakari kadhia hiyo na kutoa uamuzi wa kuunda kamati, ambao wananchi waliuridhia. 

Aliitaka kamati hiyo inayohusiaja wajumbe kutoka vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuitaka imkabidhi ripoti ndani ya siku tatu hadi Ijumaa Septemba 13, 2024 itakapokabidhi ripoti.