Wakili Chadema: Mnyika ameitwa Polisi Kinondoni

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ametakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano, Wakili wa chama hicho amethibitisha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 12, 2024 Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu amesema kiongozi huyo ameitwa na Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa kipolisi wa Kinondoni, japo hawakuambiwa anaitiwa nini.

“Ni sahihi kwamba Mnyika ameitwa. Tuliletewa taarifa kwamba anaitwa, lakini kwa sasa yupo mkoani Tabora. Nitampeleka kesho (Septemba 13, 2024),” amesema.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi alipoulizwa kuhusu wito huo, amesema hana taarifa kwa kuwa yupo nje ya kituo chake cha kazi.

Kuhusu sababu za wito huo, Wakili Mwasipu amesema hawajaambiwa, lakini wanahisi ni uchunguzi wa matukio ya utekaji.

“Kuna siku Mnyika alieleza kuwa matukio ya utekaji yachunguzwe, kwa hiyo nadhani ndio wameanza uchunguzi wao,” amesema.

Hata hivyo, Mnyika alipotafutwa kwa simu hakupokea.

Taarifa za wito wa Mnyika zilianza kusambaa jana usiku Septemba 11, 2024 baada Meya wa zamani wa Kinodnoni na Ubungo, Boniface Jacob kuandika kwenye ukurasa wake wa X akisema; “Nimetaarifiwa kuwa Jumanne Septemba 10, 2024 Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kupitia RCO Kinondoni waliwapigia simu mawakili wa Chadema kwamba wanamhitaji Katibu Mkuu, John Mnyika kwa mahojiano.”