Ninja awakosa Waangola CAF | Mwanaspoti

BEKI wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa katika timu ya FC Lupopo ya DR Congo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ameshindwa kuondoka na kikosi hicho kwenda Angola kuvaana na wababe wa Coastal Union, AS Bravos katika mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu hiyo akianika kinachombeba ugenini.

Ninja aliliambia Mwanaspoti kuwa, hajasafiri na timu hiyo kucheza mechi hiyo ya mkondo wa kwanza dhidi ya Bravos do Maquis iliyoitoa Coastal Union kwa jumla ya mabao 3-0 kutokana na kuwa majeruhi, lakini akiamini huenda akawa fiti kwa mchezo ujao wa marudiano wakiwa nyumbani DR Congo.

“Sijasafiri na timu kwa sababu niliumia goti, ila kwa sasa nimeanza mazoezi ya gym, naamini wenzangu ambao wamesafiri, watafanya vizuri na watapata ushindi katika mchezo huo, ni muhimu kushinda kwani Bravos niliwaona walipocheza na Coastal, sio wepesi hasa wakiwa kwao,” alisema Ninja.

Nyota huyo wa zamani wa Taifa Jang’ombe na Dodoma Jiji aliyewahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi katika klabu za MFK Vyskov, LA Galaxy II na Lubumbashi Sports, ameanika vitu vilivyombeba na kumudu kucheza DR Congo kwa misimu wa tatu sasa.

Ninja alisema mchezaji anayetoka nje ya DR Congo anapaswa kujifunza kuendana na mazingira, kuhakikisha analinda kiwango alichonacho vinginevyo inaweza ikala kwake na bahati nzuri yeye ameshtuka mapema.

Kauli yake ilitokana na hali ya amani ya nchi hiyo, hivyo kuna wakati ratiba zinakuwa zinaahirishwa mara kwa mara, jambo analoliona mchezaji asipojifunza mazingira hayo, anaweza akajikuta anapoteza morali ya kucheza.

“DR Congo ni tofauti na Tanzania ambayo ina amani na unaweza ukafanya kila kitu kwa uhuru, huku haipo hivyo, kitu kikubwa nilichojifunza na muhimu ni kujisimamia katika mazoezi binafsi, ambayo muda wote nitakapotakiwa kucheza mechi niwe tayari kuwajibika.