ARFA yajitosa Mbuni, TMA Stars

WAKATI Ligi ya Championship ikitazamiwa kuanza mwishoni kwa mwezi huu, Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA) kimeweka wazi kimejipanga kutoa sapoti ya kutosha kwa timu za Mbuni na TMA Stars ili zifanye vyema na kupanda daraja.

Mara ya mwisho kwa Arusha kuwa na timu ya Ligi Kuu ilikuwa ni mwaka 2014, miaka 10 iliyopita, kupitia JKT Oljoro ambayo nayo msimu huo wa 2013/14 ilishuka daraja.

Baada ya hapo mkoa huo ukajipapatua kupitia timu zake zilizokuwa Championship wakati huo ambazo ni JKT Oljoro, Arusha United na AFC Arusha kutaka kurejea Ligi Kuu lakini zikaishia kupotea kwenye ramani ya soka.

Kwa sasa Arachuga ina timu mbili za Mbuni ambayo inashiriki Championship kwa msimu wa tatu na TMA Stars ambayo ni msimu wa pili, timu zote zinamilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mwenyekiti wa ARFA, Zakayo Mjema aliliambia Mwanaspoti kuwa, kama chama wameandaa mikakati mizuri ya kuhakikisha wanazipa sapoti timu hizo ambazo anaamini itazifanya kupanda daraja na kurejesha heshima ya Arusha.

Alisema wanariadhishwa na usajili uliofanywa na timu hizo mbili kwa maana ya kusajili wachezaji wengi wenye uzoefu na Ligi ya Championship ambayo ni ngumu, hivyo sasa kazi iliyobaki ni ushirikiano ili kuzipandisha.

“Timu zote mbili ni nzuri, kikubwa wadau wazipe sapoti ya kutosha ili ziweze kupanda daraja, jambo ambalo litakuwa heshima kwetu na pia litakata kiu ya mashabiki ambao wanatamani kuona timu hizi zikipanda,” alisema Mjema na kuongeza tayari wamekutana na viongozi wa timu hizo kujadili namna gani ya kushirikiana ili kuweza kufanya vizuri na kuzipandisha daraja.

Arusha wanatarajia kuwa na uwanja mpya wa kisasa wa soka, ambao utajengwa kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, ambazo Tanzania itaandaa kwa mara ya kwanza ikishirikiana na Uganda na Kenya.