KENGOLD ilitikisa sana katika Ligi ya Championship msimu uliopita hadi ikafanikiwa kupanda kibabe katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kule Championship ilionekana kubebwa zaidi na nguvu ya fedha na ikaonekana kama ingekuja kuleta ushindani katika Ligi Kuu kwa vile wengi waliamini hali ya kiuchumi kwao haiwezi kuwa tatizo.
Hata hivyo, ilipoanza tu maandalizi ya Ligi Kuu msimu huu, ikaanza kuwapa watu wasiwasi kwamba kile ambacho wanakiamini kwa timu hiyo kipo tofauti na uhalisia.
Ikafanya usajili wa kubangaiza wa kundi kubwa la wachezaji wa kawaida huku ikiwakosa wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu ambao wangeifanya isiwe na ugeni katika ligi na pia kumudu mapema ushindani wake.
Katika hali ya kushangaza ikasajili makipa wawili wa kikosi cha wakubwa huku ikijaza kundi kubwa la wachezaji katika nafasi nyingine hasa ile ya kushambulia.
Hii ilimaanisha kuwa ikitokea kipa mmoja wa KenGold anaumia au anatumikia adhabu, timu hiyo itabaki na kipa mmoja tu wa kikosi cha wakubwa jambo ambalo ni kosa kubwa kiufundi kwa vile ikitokea naye akakosekana, timu italazimika kutumia kipa wa kikosi cha vijana ambaye huwezi kumuwekea dhamana.
Kabla suala la kusajili makipa wawili halijapoa, KenGold imeibuka na kituko kingine cha kuvaa jezi zenye wadhamini wawili tofauti ambapo fulana za juu za kampuni ya Puma na bukta za kampuni ya Nike kwenye mechi yake dhidi ya Fountain Gate, juzi Jumatano.
Inaripotiwa kwamba sababu ya kufanya hivyo ni kutokuwa na jezi mbadala baada ya bukta za jezi ambazo walipaswa kuzitumia katika mechi hiyo kufanana na zile za wenyeji Fountain Gate hivyo wakalazimika kununua bukta za rangi nyingine kwa dharura.
Inaonekana KenGold bado hawajui kama wapo Ligi Kuu kwani mambo ambayo wameanza kuyaonyesha hayaendani na hadhi ya daraja la ligi waliyopo sasa hata kwa Championship au First League.
Mbaya zaidi wameanza na umaarufu wa kuchekesha badala ya kuvuna pointi uwanjani maana hadi sasa hawana pointi hata moja katika mechi tatu walizocheza.