BAADA ya kipigo cha tatu mfululizo kwenye ligi, vimemvuruga Kocha wa Kagera Sugar, Paul Nkata akisema ubora mdogo wa wachezaji ndiyo sababu ya kushindwa kupata matokeo.
Nkata amefunguka hayo baada ya kuambulia kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tabora United na alisema timu yake haina ubora wa kushindana na timu pinzani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nkata alisema alikuwa na mchezo bora kipindi cha pili dhidi ya Tabora United lakini wachezaji wake walishindwa kumpa matokeo.
“Hadi tulipofikia sasa nafikiri kilichopo ni kwamba nina kikosi cha kawaida ambacho hakiwezi kutoa ushindani kwa wapinzani licha ya kwamba kupata matokeo ugenini sio kazi rahisi,” alisema Nkata na kuongeza;
“Kushinda ugenini sio rahisi, tumepambana lakini bahati haikuwa upande wetu, licha ya kucheza vizuri kipindi cha pili nitaendelea kupambana kuiweka timu kwenye ushindani.”
Alisema amekuwa na mwanzo mbaya lakini sio mwisho wa timu yake kuendelea kupambania nafasi ya kupata matokeo kwenye mechi zilizo mbele licha ya kukiri kuwa na kazi ngumu ya kufanya kuiweka timu hiyo kwenye ushindani.
Kagera imepoteza mechi zote tatu haijapata nafasi ya kufunga bao hata moja ikiruhusu mabao manne, imecheza mechi mbili nyumbani na moja ugenini.
Ilianza kufungwa na Singida Black Stars bao 1-0, Yanga mabao 2-0 mechi zote uwanja wa nyumbani na juzi imeambulia kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Tabora United.