Lipiki aendesha mafunzo kwa watoto

WATOTO 30 wameshiriki katika mafunzo ya Min Basketball katika Uwanja wa Ukonga, Magereza yaliyoendeshwa na Kocha wa timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 16, Denis Lipiki.

Mafunzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu 2014, yalihusisha watoto wa umri miaka sita hadi 14 na kwa mujibu wa kocha Lipiki, lengo lilikuwa ni kuwahamasisha jamii kushiriki na kuweka misingi kuanzia utotoni.

Alisema katika mafunzo hayo, waliwafundisha watoto hao jinsi ya kutoa pasi na kuzuia.

“Kwa kweli watoto walifurahi na mafunzo tuliyowapa na wengi walituomba tuweke ratiba ya kuendesha mafunzo  kila mwezi,” alisema Lipiki.

Ally Issa (10) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi ya Ukonga alisema mafunzo aliyoyapata yamemfanya aupende mchezo huo zaidi na kuahidi kutafuta viwanja kunakofanyika mazoezi ili kuendelea kujifunza.