Moshi. Rais Samia Suluhu Hassan amewapa tuzo na zawadi askari 10 waliolitumikia Jeshi la Polisi kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika, akiwamo WP namba 3, Theresia Mgaga (84).
Askari huyu alistaafu Jeshi mwaka 1990 baada ya kulitumikia kwa miaka 32.
Rais Samia ametoa tuzo hizo leo Jumanne, Septemba 17, 2024 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi nchini.
Hafla hiyo imeenda sambamba na kufunga mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, zamani CCP.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime akisoma wasifu wa WP Theresia Mgaga amesema ni miongoni mwa askari wa kike wa kwanza kujiunga na Jeshi hilo mwaka 1958. “Katika utumishi wake, aliwahi kushiriki katika upelelezi wa kesi ya wizi wa fedha za benki zilizokuwa zikisafirishwa na treni na alifanikiwa kuwakamata wahalifu na kurejesha fedha zilizokuwa zimeibwa na Mwaka 1964, alihamishiwa ofisi ya Rais Ikulu,” amesema Misime.
Amebainisha kuwa Theresia ambaye alizaliwa mwaka 1939 mkoani Tanga, alihitimu masomo yake ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Tabora mwaka 1958 na baadaye akajiunga na Jeshi la Polisi na aliandikishwa kwa namba WP 3. Misime amesema mwaka 1990 alistaafu kazi hiyo akiwa ametumikia kwa miaka 32 na sasa ana miaka 84.
Mwingine aliyepokea tuzo ni Mrakibu wa Polisi Mwandamizi Mstaafu, Abdallah Mbwana, aliyezaliwa mwaka 1931 Muheza, mkoani Tanga. Misime amesema askari huyu alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1954 na kustaafu mwaka 1975 na alishiriki kuimarisha ulinzi wakati wa siku ya uhuru wa Tanganyika na alikuwa miongoni mwa maofisa waliopewa jukumu la kulinda jukwaa kuu lililokuwa likitumika na Joshua Nkomo, mpigania uhuru wa Zimbabwe.
“Abdallah pia alihusika katika upelelezi wa mamluki wa Rhinos waliokuwa wakiingia Tanzania kuwatafuta wapigania uhuru wa Msumbiji,” amesema Misime.
Akimzungumzia Constable mstaafu wa Polisi, Protas Ngasikwa (99), amesema alizaliwa mwaka 1925 Wilaya ya Mlimba, Mkoa wa Morogoro ambaye naye amepokea tuzo yake kutoka kwa Rais Samia.
Misime anasema alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1955 na alistaafu baada ya utumishi wa muda mrefu.