Kagere: Kunifikia Bara sio rahisi

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Meddie Kagere amesema sio rahisi washambuliaji kufikia rekodi aliyoiweka akiibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo Ligi Kuu Bara kama watapambana na kivuli chake na sio kujitoa.

Wakati huohuo Kagerea ametaja pacha mbili zilizompa mafanikio ya kufanikiwa kuandika rekodi kwenye soka Bara msimu wake wa kwanza.

Kagere alifanya hivyo msimu wa 2018/19 akifunga mabao 23 na 2019/20 akafunga 22 rekodi ambayo haijafikiwa na mchezaji yeyote hadi sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo alisema sio rahisi mchezaji akaivunja rekodi hiyo kama hatajitoa na akamtazama zaidi yeye zaidi.

“Kujitoa, kufanya kazi kwa usahihi na kutomuangalia mpinzani nini anakifanya ndio siri ya mafanikio hayo na naumia pia kushindwa kuvunja rekodi yangu mwenyewe ya msimu wa kwanza,” alisema.

“Pia mafanikio hayo yalitokana na baadhi ya wachezaji ambao nilikuwa nacheza nao sambamba kuwa washambuliaji wenye jicho la kuona goli na kutengeneza nafasi. Nakumbuka nimecheza sambamba na Chris Mugalu, John Bocco na Emmanuel Okwi, ni pacha zilizochangia mafanikio yangu.”

Kagere amezitaja pacha hizo kuwa zilikuwa bora na mfano wa kuigwa kwa makocha kwani wengi hawaamini katika kuchezesha washambuliaji watatu, lakini miaka hiyo hilo lilikuwa linatokea na kutoa mafanikio.

“Fikiria tulikuwa tunacheza washambuliaji watatu na wote tunafunga haijawahi kutokea. Lakini, nilicheza na Bocco na Mugalu tulitengeneza mabao mengi na mimi kufanikiwa kuwa bora kwenye ufungaji,” alisema na kuongeza:

“Tulitengeneza pacha nzuri yenye mafanikio makubwa ndani ya Simba.”

Related Posts