KOCHA mpya wa Kiluvya United, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ amesema anahitaji muda zaidi wa kutengeneza kikosi hicho ili kilete ushindani msimu huu, huku akieleza mapungufu makubwa ya timu hiyo ni kutokuwa na maandalizi bora ya msimu ‘Pre Season’.
Kocha huyo wa zamani wa Stand United amejiunga na kikosi hicho akichukua nafasi ya Twaha Beimbaya aliyeondolewa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya timu hiyo, iliyoifanya kuburuza mkiani na pointi moja tu baada ya kucheza michezo tisa.
“Itahitaji muda ili kutengeneza timu ya ushindani kutokana na aina ya ligi tuliyopo, sio rahisi kwa sababu sehemu ambayo tupo hairidhishi, tutaendelea kupambana ila changamoto niliyoiona hapa hawakuwa na maandalizi mazuri ya msimu,” alisema.
‘Mahdi’ aliyewahi kufundisha timu mbalimbali zikiwemo Namungo, Cosmopolitan na Singida United aliongeza, kwa sasa hawana budi kupambana na hali hiyo, ingawa kikosi hicho kinahitaji maboresho zaidi wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Timu hiyo ambayo inashiriki Ligi ya Championship msimu huu, imepanda daraja baada ya kuonyesha uwezo mkubwa na kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita katika Ligi ya ‘First League’ nyuma ya mabingwa wa michuano hiyo African Sports ya Tanga.