LICHA ya Namungo kuanza msimu kwa matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu Bara, lakini kocha msaidizi wa kikosi hicho, Shadrack Nsajigwa anaamini timu hiyo ina uwezo wa kubadilika na kuwa na msimu bora zaidi ya uliopita.
Msimu uliopita Namungo ilimaliza ligi katika nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi 36.
Hata hivyo, ndani ya mechi 10 za mwanzo msimu huu, kikosi hicho kimekusanya pointi tisa.
Lakini, pamoja na changamoto hizo, Nsajigwa ana matumaini makubwa.
“Kila timu inapitia changamoto na sisi hatuko tofauti, ingawa hatujapata matokeo mazuri kama tulivyotarajia mwanzoni. Tunajitahidi kurekebisha makosa yetu,” alisema Nsajigwa.
“Tuna wachezaji wenye vipaji na benchi la ufundi lenye uzoefu. Tuna imani kwamba kwa kujituma na kuweka malengo sahihi tunaweza kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.
“Tunahitaji kushirikiana kama timu na kuhakikisha tunapata matokeo bora katika mechi zijazo.”
Namungo ilifanya mabadiliko makubwa kwenye benchi la ufundi wiki chache zilizopita, hivi sasa ikiwa chini ya kocha mkuu Juma Mgunda bado wanapambana kutafuta muunganiko bora, tayari wameonyesha dalili za kuimarika, kwani msimu uliopita baada ya mechi 10 walikuwa na pointi nane pekee.
“Ligi Kuu ni ngumu, kila timu imejiandaa kupambana. Hatuwezi kuchukulia mechi yoyote kirahisi, lakini tunaamini tunaweza kupindua hali hii. Tunawaomba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono kwani bado tuna safari ndefu ya mafanikio,” aliongeza Nsajigwa.
Mechi ijayo ya Namungo dhidi ya Mashujaa itapigwa Novemba 23, mwaka huu, mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na itakuwa kipimo kingine muhimu kuonyesha mabadiliko na kuanza kupambana kufanikisha malengo ya msimu huu.